Brazil iko tayari kwa Kombe la Dunia | Michezo | DW | 11.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Brazil iko tayari kwa Kombe la Dunia

Rais Dilma Rousseff amewaomba Wabrazil kuungana pamoja kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2014, akisema taifa liko tayari. Migomo na maandamano kuhusiana na gharama za maandalizi vinatishia tamasha hilo

Rais Rousseff amewataka Wabrazil kuwa na matumaini kuhusiana na dimba la mwaka huu la Kombe la Dunia, akisema mafanikio ya kuandaa kinyang'anyiro hicho yatauwakilisha ushindi wa ari ya taifa.

Katika hotuba yake iliyorushwa kwenye televisheni kabla ya ufunguzi wa tamasha hilo, rais huyo amesema macho ya ulimwengu mzima yanaiangazia Brazil akisema nchi hiyo ilikabiliana na changamoto kubwa na sasa iko tayari ndani na nje ya viwanja kwa ajili ya burudani hilo la soka.

Brasilien Präsidentin Dilma Rousseff mit WM-Pokal

Rais wa Brazil Dilma Rousseff ameitetea gharama ya maandalizi ya Kombe la Dunia 2014

Rousseff ameihutubia moja kwa moja timu ya taifa "selecao" akiwaambia wachezaji kwamba “katika hayo mavazi ya rangi za kijani na njano, mnadhihirisha historia ya watu wa Brazil”.

Kitisho cha migomo na maandamano

Wakati huo huo, kitisho kilichokuwepo cha mgomo kimeondolewa kwa muda huku wafanyakazi wa treni za chini ya ardhi mjini Rio wakiufutilia mbali mgomo wao baada ya kupewa nyongeza ya mshahara ya asilimia 8. Mgomo wa siku tano wa usafiri mjini Sao Paulo pia ulisitishwa Jumatatu wiki hii, ijapokuwa huenda ukarejea tena wakati michuano itakapoanza kama wafanyakazi waliopigwa kalamu hawatorudishwa kazini.

Sherehe za ufunguzi wa dimba hilo zinaandaliwa katika uwanja wa Corinthians Arena, mjini Sao Paulo, na miongoni mwa wageni watakaohudhuria ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon pamoja na viongozi 12 wa nchi na serikali.

Brasilien / Soldat / Fußball-WM

Zaidi ya wanajeshi na polisi 150,000 wataweka doria kuhakikisha usalama wakati wa dimba hilo

Lakini kabla ya kuziona timu zao zikimenyana viwanjani, mashabiki wanaowasili nchini Brazil kwanza watalazimika kupambana na mparaganyiko katika viwanja vya ndege, pamoja na foleni za taxi za hadi saa mbili. Viwanja vya ndege vinajiandaa kuwakaribisha mamilioni ya wasafiri wa kimataifa wanaotua nchini humo kwa ajili ya tamasha hilo kubwa la soka. Maafisa wa Brazil wanasisitiza kuwa watakuwa tayari, lakini abiria huenda wakajikuta katika hali ngumu. Timu zote 32 zimewasili nchini humo tayari kushuka dimbani kupambana na wapinzani.

Brazil dhidi ya Croatia

Baada ya sherehe za ufunguzi, vijana wa kocha Luiz Felipe Scolari, maarufu kama “SELECAO” watashuka dimbani kupambana na Croatia katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A. Na kama wenyeji hao wataweza kufika katika fainali na kunyakua taji hilo mnamo Julai 13, watakuwa timu ya tatu pekee iliyocheza mechi ya ufunguzi kuwahi kufanya hivyo.

Katika vinyang'anyiro 19 vya Kombe la Dunia, ni Italia pekee mnamo mwaka wa 1934 na England mwaka wa 1966 zilizowahi kucheza mechi ya kwanza na baadaye kushinda katika fainali.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo