1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brahimi kukutana na viongozi wa nchi za Kiarabu

Josephat Nyiro Charo17 Septemba 2012

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Saudi Arabia, Misri na Uturuki wanajiandaa wanakutana leo (17.09.2012) mjini Cairo nchini Misri kwenye mkutano muhimu kuhusu mzozo wa Syria.

https://p.dw.com/p/16AER
Syria's Deputy Foreign Minister Faisal Mekdad (R) welcomes United Nations (U.N.)-Arab League peace envoy for Syria Lakhdar Brahimi (L) upon his arrival at a hotel in Damascus September 13, 2012. Brahimi arrived in Syria on Thursday, his first trip to the country since taking up his post, pledging to work to end violence in which more than 27,000 people have been killed. REUTERS/Khaled al-Hariri (SYRIA - Tags: POLITICS CIVIL UNREST)
Lakhdar Brahimi alipokuwa DamascusPicha: Reuters

Mjumbe maalumu wa jumuiya ya nchi za kiarabu na wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi, atahudhuria kikao hicho cha mawaziri wa mambo ya kigeni, ambacho lengo lake kuu ni kuyakomesha machafuko ndani ya Syria. Atakutana pia na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu, Nabil al-Arabi mjini Cairo kabla ya kwenda New York, Marekani kukutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.

Brahimi atamfahamisha Arabi kuhusu ziara yake ya kwanza ya siku nne nchini Syria aliyoikamilisha jana ambapo alikutana na rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, viongozi wa serikali na upinzani na pia kuzungumza kwa njia ya simu na makamanda wa jeshi huru la nchi hiyo.

Kamanda wa jeshi huru la Syria wa mkoa wa Aleppo, kanali Abdel Jabbar al-Okaidi, ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kuwa Brahimi atashindwa kama walivyoshindwa wajumbe wengine waliomtangulia, lakini hawataki kuwa sababu ya kufeli kwake. Brahimi mwenyewe alikiri anakabiliwa na kibarua kigumu.

"Nilisema ni kazi ngumu, bado ni ngumu sana na itabaki kuwa ngumu. Nimeikubali kwa kuwa nina matumaini makubwa nitaweza kuwasaidia Wasyria hata kama ni kidogo."

Iran kutangaza msimamo wake

Wakati huo huo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Iran, Ali Akbar Salehi, anatarajiwa pia kufanya mazungumzo na rais wa Misri, Mohamed Mursi, kwenye mkutano tofauti wakati wa ziara yake mjini Cairo.

Salehi ameliambia shirika la habari la ISNA kabla kuondoka mjini Tehran mapema leo kwamba Iran itapania kutangaza wazi msimamo wake kuhusu mshirika wake Syria. Waziri huyo amesema wana matumaini makubwa kuhusu mkutano huo na kwamba matokeo yake yatalingana na masilahi ya watu wote wa eneo hilo, amani na uthabiti. Salehi amesema kufanyika kwa mazungumzo hayo ni hatua muhimu ya kutia moyo. Amesema Iran inapania kulitanua kundi la mataifa manne linalojaribu kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria, kuzijumuisha Iraq na Venezuela.

Iranian Foreign Minister Ali Akbar Salehi speaks during an interview with Reuters in Abu Dhabi July 9, 2012. REUTERS/Ben Job (UNITED ARAB EMIRATES - Tags: POLITICS HEADSHOT)
Waziri wa kigeni wa Iran, Ali Akbar SalehiPicha: Reuters

Hapo jana Jeshi la Mapinduzi la Iran lilikiri kwamba wanachama wa kikosi chake maalumu cha Quds wako nchini Syria, lakini mkuu wa jeshi hilo akathibitisha ni washauri tu na wala si sehemu ya harakati ya kijeshi.

Vikosi vya Syria vyasonga mbele

Mkutano wa mataifa yanayounda kundi la mawasiliano juu ya Syria, ambalo ni wazo la rais Mursi, unafanyika huku vikosi vya Syria vikisonga mbele katika mji wa Aleppo. Shirika la habari la serikali SANA limeripoti kuwa wanajeshi wamekidhibiti kitongoji cha Midan kaskazini mwa mji huo. Tangazo hilo linakuja baada ya wanaharakati kuripoti juu ya mashambulizi makali dhidi ya ngome za waasi kote nchini hapo jana.

Residents and members of the Free Syrian Army put out a fire caused by a jet shelling in Aleppo's district of al-Shaar September 16, 2012. REUTERS/Zain Karam (SYRIA - Tags: CONFLICT)
Shambulizi mjini AleppoPicha: Reuters

Watu wasiopungua 50 waliuwawa jana kote nchini Syria ambako wanaharakati wa upinzani wanasema vikosi vya rais Bashar al Assad vimeimarisha mashambulizi dhidi ya ngome za waasi. Kundi la kutetea haki za binadamu la Syria limesema idadi kubwa ya vifo ilitokea katika eneo lililo karibu na mji mkuu, Damascus na mji wa kaskazini wa Aleppo. Milio ya risasi na bunduki za rasharasha ilisika pamoja na milipuko katika sehemu mbalimbali za Damascus, wakati mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasi yalipopamba moto katika kitongoji cha Harasta.

Orodha ya washukiwa wa uhalifu wa kivita

Sambamba na hayo wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema leo wametayarisha orodha ya siri ya vikundi na Wasyria wanaoshukiwa kufanya uhalifu wa kivita na wanaotakiwa kujibu mashitaka siku moja. Wachunguzi hao wakiongozwa na Paulo Pinheiro wamesema wamekusanya ushahidi wa kutosha na kulihimiza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liuwasilishe mzozo wa Syria kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC, mjini The Hague, Uholanzi. Pinheiro amesema idadi ya wanamgambo imeongezeka kwa kiwango cha kutisha, wengine wakijiunga na waasi na wengine wakiendesha harakati zao wakiwa huru.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman