Bozize amtimua Waziri wa Ulinzi | Matukio ya Afrika | DW | 03.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Bozize amtimua Waziri wa Ulinzi

Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amemfukuza kazi Waziri wa Ulinzi nchini humo pamoja na Mkuu wa majeshi kutokana na kushindwa kuwadhibiti waasi wa Seleka.

Katika tangazo lililotolewa kupitia kituo cha radio cha taifa nchini humo, Rais Bozize amelikosoa jeshi kwa kushindwa kukomesha harakati za waasi kuukaribia mji mkuu wa nchi hiyo Bangui kiasi cha kufikia umbali wa kilometa 75 karibu na mji huo.

Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Waziri wa ulinzi aliyefukuzwa kazi ni mtoto wa kiume wa rais Bozize anayeitwa Jean Francis Bozize. Hatua hiyo inachukuliwa wakati waasi wa kundi la Seleka wakiwa wametangaza kusitisha harakati zao za kuelekea Bangui.

Kutokana na kuendelea kwa mzozo nchini humo Umoja wa Mataifa umetoa mwito kwa pande zote mbili kukaa katika meza ya majadiliano na kutafuta suluhu ya matatizo yao ukisema kuwa uko tayari kuyaratibu mazungumzo hayo.

Msemaji wa umoja huo, Martin Nesirky, ameliambia shirikia la habari la AFP kuwa wanaendelea kufuatilia hali ya mambo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa umakini mkubwa.

Juhudi za Umoja wa Mataifa

Naye Balozi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Margaret Vogt, yuko karibu na pande zote mbili katika taifa hilo pamoja na washirika kutoka nchi za eneo zima la Afrika ya Kati ili kuhakikisha kwamba yanafanyika majadiliano ya amani.

Rais Denis Sassou-Nguesso wa Jamhuri ya Kongo

Rais Denis Sassou-Nguesso wa Jamhuri ya Kongo

Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, mazungumzo ya amani yamepangwa kufanyika tarehe 8 Januari kwenye mji mkuu wa Gabon, Libreville, na yataratibiwa na Rais wa Jamhuri ya Kongo Brazaville, Denis Sassou Nguesso. Sassou Nguesso ndiye aliyeteuliwa kuwa kiongozi wa majadiliano ya amani katika nchi za eneo la Afrika ya Kati.

Wawakilishi wa serikali na upande wa waasi wote wamesema kuwa wamekubali kushiriki mazungumzo hayo ingawa hawajathibitisha kukubali tarehe hiyo iliyopangwa.

Waasi wakubali mazungumzo

Rais Francois Bozize na wanajeshi wake

Rais Francois Bozize na wanajeshi wake

Katika kipindi cha wiki tatu waasi wa muungano wa Seleka wameweza kuiteka miji muhimu nchini humo na sasa wako karibu na mji mkuu wa Bangui wakitishia kuutwaa wakati wowote. Waasi hao wanamtuhumu Bozize kwa kushindwa kutimiza makubaliano ya amani ya mwaka 2007.

Hapo jana waasi hao walitangaza kusitisha mashambulio yao kuelekea mji mkuu Bangui na kutuma ujumbe katika mazungumzo yanayosimamiwa na jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Afrika kati, mjini Libreville nchini Gabon.

Msemaji wa waasi, Eric Massi, alisema kwa njia ya simu kutoka Paris, Ufaransa amewataka wanajeshi wao wasisonge mbele kutoka mahala waliko hivi sasa kwa sababu wanataka kushiriki katika mazungumzo ya Libreville ili kusaka ufumbuzi wa kisiasa.

Mwandishi: Stumai George/Afp/ Reuters

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza