Borussia Dortmund yatinga nusu fainali Champions League | Michezo | DW | 10.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Borussia Dortmund yatinga nusu fainali Champions League

Timu ya Borussia Dortmund jana usiku imeandika hadhiti ya kusisimua katika uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wake, kwa kujikatia tiketi ya kucheza katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wachezaji wa Borussia Dortmund

Wachezaji wa Borussia Dortmund

Ushindi huo wa Dortmund ni wa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15. Haikuwa kazi rahisi jinsi wengi walivyotarajia kwa sababu ilibidi wazitumie dakika tatu za majeruhi kuwabandua Malaga katika hatua ya robo fainali. Mabao kutoka kwa Marco Reus na Felipe Santana yaliipa Borussia Dortmund ushindi wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya Malaga. Robert Lewandowski awali alisawazisha goli la Malaga katika kipindi cha kwanza.

Malaga ilikuwa inaongoza dhidi ya Dortmund kwa mabao mawili kwa moja hadi pale dakika tatu za ziada zilipoongezwa na ndipo Dortmund iliposawazisha kupitia Reus na kisha Santana kufunga bao jingine katika kile kilichoonekana kama ameotea.

Katika dakika ya 25 Malaga ilijipatia goli lake la kwanza kupitia mchezaji wake Joaquin, lakini goli hilo lilisawazishwa na Dortmund katika dakika ya 40 kupitia mchezaji wake, Lewandowski. Hata hivyo, timu hiyo ilikuwa ikihitaji goli zaidi ili kuweza kusonga mbele. Katika mchezo wa kwanza, timu hizo mbili zilitoka sare ya bila kufungana.

Kocha wa Dortmund azungumzia ushindi

Akizungumzia ushindi huo, kocha wa Borussia Dortmund, Juergen Klopp amesema anahisi kama tayari wamelinyakua kombe la ubingwa na kwamba ushindi wa jana usiku ulikuwa wa ajabu na hatousahau kamwe.

Kocha wa Borussia Dortmund, Juergen Klopp

Kocha wa Borussia Dortmund, Juergen Klopp

Klopp, amesema katika mchezo lazima kutakuwa na timu iliyo na bahati na timu itakayopoteza mchezo.

Chini ya kocha wake, Manuel Pellegrini, timu ya Malaga ilikuwa inajaribu kuwa timu ya kwanza kufikia hatua ya nusu fainali katika kampeni yake ya kwanza ya michuano ya ligi ya Mabingwa wa Ulaya, tangu Villar-real ilipofanikiwa kuingia nusu fainali mwaka 2006 ambapo pia ilikuwa chini ya kocha Pellegrini.

Katika mechi nyingine za robo fainali, Real Madrid walifuzu kuingia katika nusu fainali, japokuwa walishindwa katika mchuwano wa mchezo wao ugenini dhidi ya Galatasaray. Real walishindwa kwa magoli matatu kwa mawili ingawa wamefuzu kuingia nusu fainali kutokana na jumla ya magoli matano kwa matatu pamoja na yale ya mchezo wa kwanza.

Mechi za leo Jumatano (10.04.2013)

Leo, Jumatano jioni, timu ya Bayern Munich itapambana na Juventus katika mechi itakayochezwa nchini Italia. Bayern Munich iliifunga Juventus mabao mawili kwa bila nyumbani katika mchezo wa kwanza wa robo fainali. Magoli ya Bayern yalifungwa na beki wake kutoka Austria, David Alaba kabla ya Mjerumani Thomas Müller kufunga bao la pili katika uwanja wa Allianz Arena muda mfupi baada ya saa moja kukamilika.

Mchezo mwingine wa leo jioni utakuwa kati ya Barcelona na Paris St. Germain, ambazo wiki iliyopita zilitoka sare baada ya kufungana mabao mawili kwa mawili. Mabao ya Barcelona yalifungwa na Lionel Messi na Xavi. Mabao ya Paris St. Germain, yalipachikwa kimiani na Zlatan Ibrahimovic na Blaise Matuidi.

Baada ya michezo hiyo la leo kuamua ni nani washindi, mechi ya nusu fainali itachezwa siku ya Ijumaa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,DW
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza