1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia Dortmund yatamba katika Bundesliga

14 Desemba 2009

Bayern Munich yarudi kileleni .

https://p.dw.com/p/L24k
Borussia DortmundPicha: picture alliance / dpa

Ugandan Cranes ni mabingwa wapya na wa zamani wa Challenge Cup-Kombe la Afrika Mashariki na Kati.

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ,mabingwa wa Afrika, wavunja moyo katika kombe la klabu bingwa la dunia huko Abu Dhabi.

Borussia Dortmund yatamba katika Bundesliga huku kipa wa zamani wa Taifa -mlinzi wa lango la Stuttgart, Jens Lehmann, aibisha tena na atimuliwa nje ya chaki ya uwanja kwa kadi nyekundu-kisa nini ?

KOMBE LA CHALLENGE CUP:

Mabingwa wapya wa Kombe la CECAFA-Challenge Cup-Kanda ya Afrika Mashariki na Kati ni Ugandan Cranes iliowazaba Ruanda (Amavumbi) mabao 2:0.hii ni mara ya11 kwa Uganda kutwaa kombe hilo.

Katika mpambano kati ya ndugu 2:Tanzania-bara (kilimanjaro Stars) na (Zanzibar Heroes, wazanzibari walilipiza kisasi cha kuzabwa bao 1:0 na Tanzania bara hapo kabla.Zanzibar imerudi visiwani na nishani ya shaba.

TP MAZEMBE HAWIKI:

Hatima ya TP Mazembe , mabingwa wa Afrika katika Kombe la klabu bingwa la dunia:

Katika kinyan'ganyiro kinacho endelea huko Abu Dhabi, Uarabuni cha kuania Kombe la dunia la klabu bingwa, waakilishi wa Afrika, TP mazembe, wemefanya uzembe na kumvunja moyo, sio tu kocha wao mfaransa, Diego Garzitto, bali hata mashabiki wa Afrika kwa jumla:

Mazembe, iliopiga upatu na kuhanikiza kila mahala kwamba , ingewapiku mabingwa mara 6 wa Afrika ,Al Ahly ya Misri ,iliowahi kumaliza nafasi ya 3 katika Kombe hili,haikufika popote.Ilishindwa kuwika Ijumaa ilipokumbana na Pohang Steelers ya Korea ya Kusini na kuzabwa mabao 2:1.

TP Mazembe ilitamba kipindi cha kwanza tu na kutoa matumaini mbele ya mashabiki 40.000 katika Mohammed bin Zayed Stadium.Baadae lakini, ilidhihirika kuwa vishindo vya Mazembe ni vya darini vilivyokuja kuishia sakafuni.Kwani, Wakorea Kusini waliwaambia kutangulia si kufika na kwa mabao 2:1 la Mazembe,wakorea kusini waliwafunza mabingwa wa Afrika kuacha uzembe.

Kocha wa TP Mazembe , mfaransa Diego Garzitto alinukuliwa kusema baadae,

"Tuliwasili hapa tukiwa tumevinjari kabisa kushinda.Inatupasa kuzingatia msiba uliotupata hapa hii leo." -Alinun'gunika kocha huyo wa mabingwa wa Afrika.

Mazembe sasa inasubiri kucheza hapo jumatano na timu iliyoshindwa juzi Jumamosi kati ya Atlante ya Mexico na Auckland City ya New Zealand kuania nafasi ya 5.

BUNDESLIGA:

Katika Bundesliga: mabao 2 maridadi ajabu ya kipindi cha kwanza aliotia muargentina Lucas Barrios, yaliongeza misiba kwa mabingwa wa Ujerumani, VFL Wolfsburg wakati huu pale Borussia Dortmund mwishoe, kuwatimua nje mabingwa hao kwa mabao 3:1nyumbani jana.

Mabingwa Wolfsburg, waliotimuliwa wiki iliopita nje ya Champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya na Manchester United,hawakuwa na jibu la hujuma za Mmisri,Mohammed Zedane katika lango lao.Ni yeye alietayarisha mabao yote 2 kati ya mabao 3 katika lango la Wolfsburg.

Kocha wa Borussia Dortmund , Jürgen Klopp,aliueleza hivi mpambano wa jana :

"Ushindi wetu ulistahiki mno.Tulikuwa timu bora. Timu yangu ilicheza kwa mbinu za ustadi mkubwa na magoli yalikuwa maridadi kabisa."-alisema Jürgen Klopp.

Msiba hasa uliangukia VFB Stuttgart na kipa wao Jens Lehmann.Baada ya kuongoza kwa bao 1:0 dhidi ya Mainz ,hadi dakika ya 90 ya mchezo, kipa huyo wa zamani wa Taifa ,alimchezea ngware mshambulizi wa Mainz Aristide Bance kwa kumpiga bega na kumtimba mguuni.Rifu akamuonesha Lehmann kadi nyekundu na bao la penalty likasawazisha kwa Mainz bao 1:1.Stuttgart ikiwa mkiani mwa Ligi kama Hertha Berlin, ilihitaji pointi zote 3 . Ikihisi imeshazitia mfukoni, Lakini, kipa wao Lehmann, aliwatilia kitumbua chao mchanga dakika ya mwisho.

Hivi ndivyo shabiki mmoja alivyo stushwa na tabia ya kipa Lehmann :

"Mchezaji ambae tabia yake si nzuri hadharani na kila mara anawa chokoza wenzake , hiyo si tabia nzuri kispoti-fair play.......Na sasa anapotamba namna hiyo, ni dalili kwamba, wakati wake umewadia kuacha kucheza mpira."

Uongozi wa viongozi wa Bundesliga-Bayer Leverkusen nao ulipunguzwa hadi pointi 1 kileleni.Leverkusen, ilimudu sare mabao 2:2 na Berlin.Schalke, ilikomesha mlolongo wa Werder Bremen wa kutoshindwa mapambano 23 mfululizo walipowazaba mabao 2:0 ili kujiweka wao nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi. Bayern Munich iliishikisha adabu Bochum kwa kuwachapa mabao 5:1 na sasa Munich inanyatia kilele kutoka nafasi ya 3.

Katika Premier League, Chelsea na mabingwa Manchester united, zote mbili ziliteleza nyumbani mwishoni mwa wiki:

Chelsea, ilimudu sare mabao 3:3 na Everton, licha ya mabao 2 ya Didier Drogba na Manu iliopo nafasi ya pili ya ngazi ya Premier League, ilikandikwa bao 1:0 na Aston villa.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman