1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson anajiandaa kuitisha uchaguzi?

Amina Mjahid
2 Septemba 2019

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinasema Waziri Mkuu wa nchi hiyo Borris Johnson anajitayarisha kuitisha uchaguzi ikiwa ni siku moja kabla ya kikao cha kujadili Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/3OtbQ
Boris Johnson
Picha: Reuters/D. Martinez

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinasema Waziri Mkuu wa nchi hiyo Borris Johnson anajitayarisha kuitisha uchaguzi ikiwa ni siku moja kabla ya kikao cha kihistoria bungeni kujadili suala la Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit. 

Ahadi ya Waziri Mkuu Borris Johnson ya kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31 ama kwa makubaliano au bila makubaliano na kutengana kati ya taifa hilo la tano kiuchumi duniani, pamoja na mshirika wake mkubwa wa kibishara imeisogeza Uingereza kwenye kingo za mgogoro mubwa wa kisiasa na mgongano kati ya wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya.

Muungano wa wabunge wa upinzani wanapanga pamoja na wapinzani ndani ya chama tawala cha Conservative chake Borris Johnson kuchukua udhibiti wa bunge na kuifunga mikono  ya serikali kupitia msuada wa kisheria utakaozuwia nchi hiyo kuondoka bila ya makubaliano wakihofia kufanya hivyo kutakuwa na matokeo mabaya.

Wabunge wa Conservative waonywa kutopiga kura dhidi ya serikali

Ikiwa ni chini ya saa 24 ya bunge kurejelea vikao vyake hapo kesho Jumanne, baada ya mapumziko ya kipindi cha kiangazi, watendaji wa Johnson wamewaonya wabunge wa Conservative wanaopanga kupiga kura dhidi ya serikali kwamba watafukuzwa chamani.

Johnson alitarajiwa kukutana na aliyekuwa waziri wa Sheria David Gauke anayepinga Brexit isiyokuwa na makubaliano

Großbritannien London Jeremy Corbyn im Unterhaus
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour nchini Uingereza Jeremy Corbyn Picha: Reuters

Hata hivyo haijawa wazi iwapo bunge litaweza kweli kuja na suluhisho ya mgogoro wa miaka mitatu wa Brexit uliyogeuka kuwa uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa mapema. Kuhusiana na hilo kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Jeremy Corbyn amesema ni lazima watu waungane dhidi ya mpango wa kuondoka bila makubaliano na kwamba chama chake kinafanya kazi na wanachama wa vyama vingine kufanya wawezalo ili kuiondoa nchi hiyo ya katika hatari ya kuondoka Umoja wa Ulaya bila makubaliano.

Lakini kwa upande wake Waziri mkuu wa Zamani wa Uingereza Tony Blair amemuonya Corbyn kuachana na kile alichokiita "mtego wa ndovu” uliowekwa wazi na Borris Jonson kwa chama chake.

Tony Blair amesema Boris Johnson anafahamu kuwa suala la Brexit bila makubaliano likisimama lenyewe linaweza kushindwa lakini akilichanganya na swali la Corbyn katika uchaguzi mkuu anaweza kufanikiwa licha ya wengi kupinga Brexit bila makubaliano, kwa sababu baadhi wanaweza wakahofia zaidi uwaziri mkuu wa Corbyn.