Bolivia kuufunga Ubalozi wa Marekani? | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bolivia kuufunga Ubalozi wa Marekani?

Rais wa Bolivia, Evo Morales ametishia kuufunga ubalozi wa Marekani nchini Bolivia kutokana na kiongozi huyo kudai kuwa nchi hiyo ilihusika kuizuia ndege yake kupita kwenye anga ya nchi kadhaa za Ulaya.

Rais wa Bolivia, Evo Morales

Rais wa Bolivia, Evo Morales

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kushuku kwamba Edward Snowden, aliyevujisha taarifa za siri za kijasusi za Marekani, yumo ndani ya ndege hiyo. Akizungumza katika mji wa Cochabamba nchini Bolivia, Rais Morales ameituhumu Marekani kwa kuyashinikiza mataifa kadhaa ya Ulaya kuzuia anga zao na kutoiruhusu ndege yake kupita.

Amesema Bolivia iko huru na ina hadhi yake, na kwamba hata bila Marekani, nchi hiyo itasimama imara kisiasa na kidemokrasia, hivyo hawauhitaji ubalozi wa Marekani. Rais Morales aliwasili nchini kwake Jumatano iliyopita, akitokea Vienna, Austria, baada ya ndege yake kuzuiwa kupita kwenye anga ya mataifa manne ya Ulaya na kulazimishwa kwenda Austria.

Edward Snowden

Edward Snowden

Kiongozi huyo amesema kuwa kitendo hicho ni sawa na kukiuka sheria ya kimataifa. Morales alikuwa akitokea Urusi, ambapo akiwa nchini humo, alisema nchi yake itayafikiria maombi ya Snowden ya kupewa hifadhi ya ukimbizi nchini Bolivia.

Viongozi wa Amerika ya Kusini wakutana

Kufuatia hatua hiyo, viongozi wa mataifa ya Amerika ya Kusini walikutana mjini Cochabamba kuzungumzia tukio hilo. Katika mkutano huo wa dharura na Rais Morales, marais wa Venezuela, Argentina, Ecuador, Uruguay na Surinam, wamezitaka nchi za Ulaya zilizohusika ambazo ni Uhispania, Ufaransa, Italia na Ureno, kuomba radhi kutokana na kitendo hicho walichokifanya. Viongozi hao wamesema kuwa kitendo hicho ni tusi kwa Bolivia na Amerika ya Kusini kwa ujumla, ambayo imeshuhudia mapinduzi kadhaa ya kijeshi yaliyoungwa mkono na Marekani.

Viongozi wa nchi za Amerika ya Kusini

Viongozi wa nchi za Amerika ya Kusini

Kabla ya kuanza kwa mkutano wao, Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, alidai kuwa Shirika la Kijasusi la Marekani-CIA iliziamuru nchi hizo za Ulaya kuizuia ndege ya Morales kupita katika anga zao. Aidha, Rais Maduro amenukuliwa akisema kuwa mmoja wa mawaziri katika nchi hizo za Ulaya, aliwaambia viongozi hao wa Amerika ya Kusini kwa njia ya simu kwamba wataomba radhi kutokana na tukio hilo. Kwa mujibu wa Maduro, waziri huyo amesema pia wao wenyewe walishangazwa na hatua hiyo na kwamba waliotoa amri hiyo kwa mamlaka ya shirika la ndege la nchi yake, walikuwa ni CIA.

Hata hivyo, Waziri wa masuala ya kigeni wa Uhispania, Jose Manuel Garcia-Margallo, amesema nchi yake haikumzuia Morales kutua kwenye ardhi yake. Viongozi hao wa Amerika ya Kusini wamesema kwa pamoja wataendelea kupambana dhidi ya ubeberu unaofanywa na Marekani. Serikali ya Morales imekuwa katika uhusiano usio mzuri na Marekeni, ambapo mwaka 2008 Bolivia ilimfukuza balozi wa Marekani nchini humo pamoja na maafisa wa shirika la kupambana na madawa ya kulevya la Marekani kutokana na hatua yao ya kuwachochea wapinzani. Hadi sasa, serikali ya Marekani imekataa kuzungumzia iwapo ilihusika katika hatua ya kuzuia anga ya nchi hizo za Ulaya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ APE,AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com