Boko Haram yaushambulia mji wa Damaturu | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Boko Haram yaushambulia mji wa Damaturu

Miripuko na milio ya risasi imeukumba mji wa Damaturu kaskazini mwa Nigeria hii leo katika shambulizi linaloaminika kufanywa na waasi wa Boko Haram linalowalenga polisi.

Mkaazi wa mji wa Damaturu Umar Sada amesema wameamshwa leo alfajiri na milio ya risasi na miripuko katika jimbo la Yobe na wameyatoroka makaazi yao na kukimbilia vichakani kwani hawajui kinachojiri ila ameongeza kambi ya polisi imeharibiwa katika shambulizi hilo.

Hayo yanakuja wakati asasi kuu ya kiislamu nchini Nigeria Jama'atu Nasri Islam JNI ikiwashutumu viongozi wa Nigeria kwa kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya Boko Haram na kuwataka waislamu nchini humo kuchukua hatua muafaka kujilinda.

Boko Haram yazidi kunoa makali

Hii ni kufuatia mashambulizi mabaya yaliyofanywa na waasi wa Boko Haram Ijumma katika msikiti ambayo yaliwaua kiasi ya watu 120 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 270 katika mji wa Kano kaskazini mwa Nigeria.

Maafa baada ya mashambulizi ya Boko Haram mjini Kano

Maafa baada ya mashambulizi ya Boko Haram mjini Kano

Kiongozi wa ngazi ya juu wa kidini ya kiislamu wa pili kimadaraka nchini Nigeria Muhammad Sanussi wa pili wiki mbili zilizopita pia alitoa wito kama huo wa kuwataka waislamu kuchukua silaha na kupambana na Boko Haram baada ya serikali kuonekana kushindwa kufanya hivyo.

Asasi hiyo ya kiislamu JNI iliyo na makao yake mjini Kaduna na inayoongozwa na Sultan wa Sokoto imewataka maafisa wa Nigeria kuonyesha nia yao ya kulinda maisha ya wanigeria na mali zao.

Asasi hiyo pia imesema hali ya hatari iliyotangazwa na serikali katika majimbo matatu ya kaskazini mwa Nigeria Yobe, Borno na Adamawa imeshindwa kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram na hatua hiyo haijakuwa na maana.

Jeshi lakosolewa

Jeshi la Nigeria limekosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na uasi huo ambao umesabisha vifo vya zaidi ya watu 13,000 tangu kuanza mwaka 2009.Sanussi wa Pili ameapa waislamu hawatatishwa na mashambulizi ya Boko Haram kuacha imani yao.

Papa Francis alaani mashambulizi ya Boko Haram

Papa Francis alaani mashambulizi ya Boko Haram

Jumuiya ya kimataifa imelaani vikali mashambulizi hayo ya Boko Haram ambayo yamesababisha hofu,uharibifu wa mali,vifo na kusababisha maelfu ya watu kutoroka makaazi yao.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameyataja mashambulizi hayo kama dhambi kubwa dhidi ya Mungu huku Rais wa Ufaransa Francois Hollande akitaka kuwepo juhudi za pamoja kukabiliana na kitisho hicho cha Boko Haram nchini Nigeria.

Boko Haram imeongeza mashambulizi na kuyanoa zaidi makali yake huku ikiendelea kuidhibiti miji na vijiji kadhaa kaskazini mashariki mwa Nigeria ambako imetangaza dola la kiislamu.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com