Bodi za uongozi ngóme ya wanaume? | Magazetini | DW | 31.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Bodi za uongozi ngóme ya wanaume?

Wito wa kuwepo kiwango fulani cha wanawake katika mabodi ya uongozi katika makampuni makubwa ya Ujerumani ni mada kuu katika magazeti ya Ujerumani leo hii.Basi utaanza na gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linalosema:

Haitoshi tu kuyaachilia makampuni yenyewe kujiamulia kiwango cha wanawake watakaoajiriwa katika ngazi za juu za uongozi. Hata mazingira ya kijamii yanapaswa kuzingatiwa. Kutahitajiwa nafasi za kutosha za kuwatunza watoto wadogo. Vile vile, liwe ni jambo la kawaida kwa wanaume kushughulikia zaidi familia na kazi za nyumbani. Na mtindo wa kuwalipa mishahara tofauti, wanaume na wanawake wenye ujuzi na shahada zinazolingana, ukomeshwe. Njia ya kuelekea huko imeshafunguliwa lakini hiyo ni njia ndefu.

Na gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG linaeleza hivi:

Daraja ya juu ya uongozi katika makampuni makubwa kabisa ya Ujerumani ni kama jamii iliyotengwa kwa ajili ya wanaume tu. Na hali hiyo itabakia hivyo hivyo. Kwani mpango uliopendekezwa na waziri wa masuala ya familia wa Ujerumani Kristina Schröder kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za juu, hatua kwa hatua, wala hautosaidia kuleta mabadiliko.

Lakini gazeti la ESSLINGER ZEITUNG likiamini kuwa mageuzi yapo njiani linasema:

Kuna ishara kuwa makampuni hayo makubwa ya Ujerumani hatimae yametambua kuwa wakati umebadilika, kwa hivyo safari hii makampuni hayo yanadhamiria kuongeza kwa kiwango kikubwa, idadi ya wanawake katika mabodi ya usimamizi. Sasa serikali yapaswa kuhakikisha kuwa makampuni hayo yatawajibika ipasavyo.

Mada nyingine iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo Alhamisi ni mzozo wa Libya. Gazeti la BADISCHE ZEITUNG linaeleza hivi:

Kuzuia mauaji ya umma kwa kutoa msaada kutoka angani ni jambo moja. Kuyapa silaha makundi ya wapiganaji waliokusanyika ni jambo tofauti kabisa. Bila shaka silaha zilizo mikononi mwa waasi zinaweza kuulinda umma dhidi ya ukatili wa Gaddafi. Lakini ukweli ni kwamba tafsiri hiyo imepindukia Azimio1973 la Umoja wa Mataifa. Kwa hivyo, kuna hatari ya kufifia kwa uungaji mkono wa kimataifa kuhusu operesheni ya Libya.

 • Tarehe 31.03.2011
 • Mwandishi Martin,Prema/DPA
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/REBm
 • Tarehe 31.03.2011
 • Mwandishi Martin,Prema/DPA
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/REBm