1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobs 2014: Piga kura!

2 Aprili 2014

Mwaka huu pia ulimwengu wa blogu umeendelea kutanuka. Kuanzia tarehe 2 Aprili, mtumiaji anaweza kupiga kura moja kwa moja.

https://p.dw.com/p/1BZeG
The Bobs Award 2014

Mwaka huu pia ulimwengu wa blogu umeendelea kutanuka. Kwa mara nyengine tena, mashambulizi dhidi ya waandishi wa blogu na waandishi wa habari pamoja na udhibiti wa serikali umewakwaza wanaharakati hao wa mtandaoni.
Suala la Shirika la Usalama la Marekani (NSA) nalo limewafanya waundaji programu kuchukuwa hatua ya kutengeneza mitando salama zaidi ya mawasiliano na teknolojia zenye uhakika.

Maandamano yaliyoanza katika majira ya kiangazi yaliyomalizika nchini Uturuki bado yangalipo hadi sasa. La juu kuliko yote ni kile kilichofahamika kama Msimu wa Mapukutiko wa Ukraine, dhana inayowakilisha mapinduzi ya umma nchini Ukraine. Na bado, ni mabara ya Afrika na Asia ndiyo yanayoongoza kwenye uvumbuzi mpya wa kiteknolojia unaowawezesha watu kupata taarifa.

Shida ziwapatazo wanablogu

Ni kawaida ya tuzo za BoBs kutolewa kwa blogu, mitandao na kampeni zilizoanzishwa na watu ambao kwenye nchi zao wanatishwa kwa hatua za kikandamizaji, mashitaka na jela. Intaneti huwa ndiyo uwanja wa mwisho ulio huru kwao.

Ama iwe ni kwa wapiganiaji wa haki za wanawake Arabuni au wapinzani nchini China, aghlabu wengi wao huishi kwenye mazingira ya udhibiti mkali na mbinu za ufungiaji Intaneti. Serikali zao zinawaandama kila wendapo, na mara kadhaa baina yao na serikali hizo huwa ni mchezo wa kuviziana na kutegana.

Katika historia ya miaka 10 ya BoBs imetokezea si mara moja wala mbili kwa walioteuliwa kupigania tuzo hizo kutoweka ghafla. Na sio wao tu, hata washindi wa hivi karibuni wa tuzo hiyo wamekamatwa.

Raia wa Cuba, Yoani Sanchez, alitekwa nyara, kupigwa na hata kutishiwa maisha yake kwa sababu ya ripoti zake zinazokosoa kwenye blogu yake “Generation Y” inayohusu maisha ya kila siku nchini Cuba, ambako utawala wa Castro unabana kila kitu. Tangu aliposhinda tuzo ya BoBs mwaka 2008, ilikuwa ni mwaka jana tu alipoweza kupokea zawadi hiyo, kwani kwa miaka yote huko nyuma alikuwa amepigwa marufuku kusafiri.

Mapendekezo

Zaidi ya mapendekezo 3,000 yaliwasilishwa, ambapo jopo la kimataifa lenye majaji 15 sasa linapaswa kuamua. Jumla ya vigawe 20 vimewekwa kwa blogu zilizoandikwa kwenye lugha 14 duniani, kuanzia Kiindonesia hadi Kifursi na Kiukraini. Jukumu la majaji ni kupitia maoni ya waliozipigia kura kuamua ni blogu ipo iliyokuwa bora zaidi kwenye kampeni zake za mtandaoni.

Baadhi ya blogu zilizoteuliwa ni kampeni ya mtandaoni iitwayo “To lae para Snowden”, inayotetea ombi la kupatiwa hifadhi nchini Brazil kwa mvujishaji siri wa NSA, Edward Snowden. Zaidi ya watu milioni moja tayari wameshasaini kwenye kampeni hiyo.

Kuna pia “Lantern” ambayo ni nyenzo ya mtandaoni kukabiliana na udhibiti wa serikali na vyombo vyake. Mtu anayejiunga na mtandao huo, basi komyputa yake inakuwa inafanya kazi kama mtoaji wa huduma ya mtandao na hivyo haiwezi kufikiwa na mitandao ya serikali ya kuidhibiti.

Ukurasa wa Facebook uitwao Euromayda nao pia umo kwenye mashindano. Huu ulikuwa chanzo muhimu kwa taarifa za yale yanayojiri nchini Ukraine. Ndani ya muda mfupi baada ya kuanzishwa kwake, ulikuwa na watu 300,000 wanaoufuatilia.

"Emmabuntus" ni programu ya kijamii iliyotengenezwa Ufaransa kwa ajili ya kukusanya vyombo vichakavu vya kompyuta na kuvitengeza kompyuta mpya kwa ajili ya mataifa masikini.

Vile vile, imeteuliwa mitandao ya kuchekesha kama vile "Thug-notes", ambayo huwa na vidio fupi za "hip-hop" zinazoelezea fasihi duniani kwa njia rahisi ambayo hadhira inaweza kuzifahamu.

Blogu na kampeni zote zilizoteuliwa zinapatikana kwenye kiungo hiki: http://www.thebobs.com:thebobs.com. Kuanzia tarehe 2 Aprili, mtumiaji anaweza kupiga kura juu yake moja kwa moja.

Mwandishi: Silke Wünsch/DW Kultur
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
.