1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yapitisha azimio kuunga mkono Kombe la Dunia 2018

27 Julai 2015

Rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Sepp Blatter amemhakikishia rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba nchi hiyo itakuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2018

https://p.dw.com/p/1G5RD
FIFA WM 2018 Russland Blatter und Putin
Picha: picture-alliance/dpa/M. Shipenkov

FIFA imepitisha azimio linalotoa ushirikiano kamili kwa Urusi kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2018 nchini Urusi. Blatter ameyasema hayo katika mkutano na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Kashfa kubwa ya rushwa inayofanyiwa uchunguzi na Marekani , Uswisi na mashirika mengine yanayolinda sheria imeitumbukiza FIFA katika mzozo mkubwa kabisa katika historia yake ya miaka 111 na kuweka kiwingu katika fainali zijazo za kombe la dunia nchini Urusi na Qatar, lakini maafisa wa Urusi wamepuuzia maelezo kwamba Urusi inaweza kuvuliwa uenyeji wa mashindano hayo.

Katika kupanga makundi ya timu kuwania kucheza katika fainali za mwaka 2018 nchini Urusi siku ya Jumamosi Uhispania na Italia zimewekwa katika kundi moja , pamoja na Uholanzi na Ufaransa, lakini mabingwa watetezi Ujerumani wamepata kibatua rahisi kidogo, ambapo itakuwa pamoja na Jamhuri ya Cheki, Ireland ya kaskazini , Norway, Azerbaijan na San Marino.

FIFA Qualifikation WM 2018 Russland Auslosung
Droo ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 UrusiPicha: Getty Images/S. Botterill

Uingereza ambayo imeweza kupata ubingwa mara moja tu mwaka 1966 , lakini imekuwa mshirika wa kawaida katika fainali hizo , inaonekana kuwa itafanikiwa baada ya kuwekwa katika kundi moja na mahasimu wao wa jadi Scotland katika kundi F. Katika kundi hilo pia zipo timu za Slovakia, Slovenia, Lithuania na Malta.

Katika bara la Afrika Cameroon italazimika kupitia vikwazo vyenye utata kidogo wakati itakapokutana ama na Somalia ama na Niger mwanzoni mwa kampeni yake kucheza katika fainali hizo. Somalia na Niger zitakutana katika duru ya awali na mshindi atacheza na Simba hao wa nyika katika michezo miwili katika duru ya pili ya michuano hiyo ya mtoano.

Sudan kusini , ambayo imejiunga na FIFA mwaka 2012, inakumbana na Mauritania katika mchezo wao wa kwanza kabisa wa kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia , ambapo itacheza mchezo wa kwanza mjini Juba. Mshindi atacheza na Tunisia katika duru ya pili ya mtoano.

Nigeria itaumana na Djibouti ama Swaziland katika duru ya pili na mabingwa wa Afrika Cote D'ivoire watalazimika kupambana na Liberia ama Guinea - Bissau.

Chung Mong-joon kutoka Korea ya kusini , ambaye anatarajiwa kutangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA mwezi ujao, amekutana na mwenzake ambaye huenda wakapambana katika kinyang'anyiro hicho cha urais Michel Platini nchini Marekani jana Jumapili na kutoa wito wa kushindana kwa busara, iwapo ataingia katika mbio hizo za kuwania kuwa rais wa FIFA.

Makamu huyo wa zamani wa FIFA Chung amesema wiki iliyopita kwamba bado anapima kutangaza nia yake ya kuchukua nafasi ya Sepp Blatter kama mkuu wa shirikisho hilo lililokumbwa na kashfa tele na kwamba anafikiria bado kutangaza nia yake hiyo katikati ya mwezi Agosti.

Chung ambaye ni tajiri mkubwa akimiliki shirika kubwa la Hyundai nchini Korea ya kusini na mmoja kati ya watu wenye ushawishi mkubwa katika soka barani Asia, ameweka picha ya mkutano wake na rais wa shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA Platini katika tovuti yake rasmi na kusema anapanga kukutana nae tena katika bara la Ulaya mwezi Agosti.

Mwandishi: Sekione Kitojo/AFP/DPA
Mhariri: Joephat Charo