1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Black Stars waaga Kombe la Dunia

3 Julai 2010

Pale mkwaju wa penalty wa Asamoh Gyan katika dakika ya mwisho ya kipindi cha ziada ulipopaa juu ya lango la Uruguay.....ilikuwa kama msumari wa moto katika nyoyo za Ghana na Afrika kwa jumla.

https://p.dw.com/p/O9hZ
Ghana's Asamoah Gyan, right, misses on a penalty shot as Uruguay goalkeeper Fernando Muslera, bottom left, looks up during the World Cup quarterfinal soccer match between Uruguay and Ghana at Soccer City in Johannesburg, South Africa, Friday, July 2, 2010. (AP Photo/Luca Bruno)
Asamoah Gyan wa Ghana (kulia) akikosea mkwaju wa penalty wakati wa robo fainali ya Kombe la Dunia, uwanjani Soccer City mjini Johannesburg, Julai 2,2010.Picha: AP

Gyan ambaye goli lake safi dhidi ya Marekani liliwafikisha Black Stars katika robo fainali ya dimba hili la kombe la dunia- alikuwa nusura aandike historia nyingine- kuwaingiza Ghana katika nusu fainali.

Uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg ulianikizwa na milio ya vuvuzela pale Sulley Muntari alipofunga bao la kwanza la Ghana katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza. Black Stars walikuwa wameanza vyema wakipania kuvunja historia kuwa timu ya kwanza kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia.

Ghana goalkeeper Richard Kingson, left, and Uruguay's Diego Forlan go for the ball during the World Cup quarterfinal soccer match between Uruguay and Ghana at Soccer City in Johannesburg, South Africa, Friday, July 2, 2010. (AP Photo/Themba Hadebe)
Kipa wa Ghana,Richard Kingson (kushoto)na Diego Forlan wa Uruguay.Picha: AP

Lakini Uruguay mabingwa mara mbili wa dunia- walirejea kwa kishindo na nyota wao Diego Forlan, akasawazisha katika dakika ya 55. Huku muda ukiyoyoma na mikwaju ya penalti ikinukia- Afrika ikapumua na kuingia matumaini pale Luis Suarez alipotumia mkono kuzuia bao la pili la Ghana ambalo lilikuwa liwafungishe virago Uruguay.

Saurez alipewa kadi nyekundu na Asamoh Gyan alikabidhiwa jukumu la kufunga penalti- ambayo kama ingeingia basi Ghana ingekuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika semi fainali. Ghana baadaye ilipoteza mikwaju miwili ya penalti- na Uruguay ikajikatia tiketi yake ya nusu fainali.

Mjini Accra- barabara za mji huo- zilikuwa tupu muda mfupi tu baada ya Black Stars kushindwa katika mikwaju ya penalti. Raia waliokusanyika katika mikahawa kuitizama mechi hiyo, nchini humo ingawa walivunjika moyo, walisema wanajivunia jinsi Black Stars walivyoonyesha ustad´i na uchezaji mzuri katika dimba hili la dunia.

"Ni hali ya kabumbu" wengine walisikika wakisema - "leo haikuwa bahati yetu" - ndio msemo ulioenea nchini Ghana na Afrika nzima- ama kweli Black Stars walikuwa wamebeba matumaini ya bara zima- ambalo kwa mara ya kwanza lilikuwa na matumaini pengine wakati wetu ni sasa- kufika angalau semi fainali za kombe la dunia.

Na kama mechi hiyo katika uwanja wa Soccer City ilikuwa ya aina yake- robo fainali ya kwanza iliwaacha wengi mdomo wazi pale mabingwa mara tano Samba wa Brazil walipoonyeshwa kidumbwedumbwe na Uholanzi. Wesley Sneijder ndie alikuwa nyota wa Uholanzi huku Felipe Melo akiwa donda sugu wa Brazil.

Netherlands' Wesley Sneijder celebrates after scoring a goal during the World Cup quarterfinal soccer match between the Netherlands and Brazil at Nelson Mandela Bay Stadium in Port Elizabeth, South Africa, Friday, July 2, 2010. The Netherlands won 2-1 (AP Photo/Frank Augstein)
Wesley Sneijder wa Uholanzi, baada ya kutia goli lililowafungisha virago Brazil.Picha: AP

Sneijder ndie aliepiga pasi safi ambayo Melo aliingiza katika wavu wa Brazil- kuisawazishia Uholanzi baada ya Robinho wa Brazil kutia bao la kwanza. Sneijder baadaye alifunga bao la pili la Uholanzi ambalo lilitosha kuwafungisha virago Brazil.

Cocha Dunga ambaye ameiongoza Brazil kwa miaka minne- alitangaza kwamba muda wake madarakani umemalizika baada ya vijana hao wa Samba kuyaaga mashindano ya Kombe la Dunia katika robo fainali.

Ilikuwa raha kwa Uholanzi ambao walishindwa na Brazil mara mbili katika kombe la dunia. Mwaka wa 1994 Brazil iliitimua Uholanzi katika raundi ya pili ya dimba- miaka minne baadaye Uholanzi tena ikapata kichapo kutoka kwa Brazil katika robo fainali. Na leo, Uholanzi ilikuwa na miadi ya kulipa deni.

Sasa Uholanzi itakutana na Uruguay jumanne ijayo katika nusu fainali ya kwanza. Leo ni zamu ya Ujerumani na Argentina na mabingwa wa Ulaya - Spain wana miadi na Paraguay- nafasi mbili za nusu fainali zitajazwa usiku huu baada ya mechi hizi mbili.

Mwandishi: Munira Mohamed/RTRE