1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bintiye kasisi ashinda tena Ujerumani

27 Septemba 2009

Angela Merkel alizaliwa kama Angela Dorotea Kasner mnamo Julai 17 mwaka 1954 mjini Hamburg katika iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Babake aliitwa Horst Kasner na alikuwa mchungaji wa kanisa la Kiluteri.

https://p.dw.com/p/JqBr
Mshindi wa uchaguzi Kansela Angela Merkel,CDUPicha: AP

Uchaguzi mkuu umekamilika Ujerumani hii leo Septemba 27. Kwa mara ya nne kansela Merkel ameorodheshwa kuwa mwanamke mwenye nguvu kubwa duniani na jarida la kiuchumi la Forbes nchini Marekani, na ni Mjerumani pekee katika orodha ya watu 100 uliwenguni.

Angela Merkel alizaliwa kama Angela Dorotea Kasner mnamo Julai 17 mwaka 1954 mjini Hamburg katika iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Babake aliitwa Horst Kasner na alikuwa mchungaji wa kanisa la Kiluteri. Mamake aliitwa Herlind Jentzsch na alikuwa mwalimu wa lugha ya Kiingereza na Kilatin.

Ndoa ya Kwanza

Mnamo mwaka 1977 Angela Dorotea Kasner aliolewa na mwanafunzi wa Fizikia, Ulrich Merkel, na hivyo kubadilisha jina lake na kuitwa Angela Dorotea Merkel. Ndoa hiyo ilimazikia na talaka mnamo mwaka 1982. Mume wake wa pili, Joachim Sauer, ni mwanakemia na profesa.

Angela Merkel mit Ehemann Joachim Sauer
Kansela na mumewake wa pili Joachim SauerPicha: dpa - Bildfunk

Novemba 22 2005 Angela Merkel alikula kiapo kuwa kansela mpya wa Ujerumani, na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo. Muongo mmoja na nusu kabla, katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki, DDR, kansela Merkel alijisajili katika kundi la upinzani la kanisa la kiinjili kama mtaalam wa sayansi ya kimaumbile. Waziri mkuu wa kwanza wa Ujerumani Mashariki kuchaguliwa katika uchaguzi huru, Lothar de Maiziere, alimteua Angela Merkel kuwa makamu msemaji wa serikali. Baada ya uchaguzi wa ukansela mwishoni mwa mwaka 1990, Merkel alipendekezwa kwa Kansela Helmut Kohl. Ambaye alimteua Angela Merkel kuwa waziri wa wanawake na vijana. Angela Merkel alifanya kazi katika ngazi ya juu ya chama chake na baadaye mwaka 2005 akachaguliwa kuwa kansela. Merkel mwenyewe alisema

"Kwamba mtu kama mimi, mwanamke kutoka iliyokuwa Ujerumani Mashariki, naweza kuwa kansela wa Ujerumani, hilo kwangu baada ya miezi 10 tangu kuingia madarakani, limekuwa jambo la kawaida. Kwa upande mwingine katika siku kama hii ya leo, ni jambo lengine la kipekee."

Nia yatimia

Ukweli ni kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2005 nia ya kuwa na serikali ya muungano wa vyama vya CDU na CSU pamoja na chama cha kiliberali cha FDP, haikutimia. Lakini hata hivyo chama cha Social Democratic, SPD, kilichounda serikali pamoja na muungano wa vyama vya CSU na CSU, kilishirikiana vizuri na kansela Merkel. Ili kuweza kupunguza deni kubwa lililoikabili nchi, serikali ya mseto iliongeza kodi ya mauzo kwa asilimia tatu, uamuzi ambao kwa chama cha SPD ulikuwa mgumu kuukubali.

Deutschland Streit um Hans Filbinger Ministerpräsident Günther Oettinger
Waziri mkuu wa jimbo la Baden-Wuttenberg Günther ÖttingerPicha: AP

Mchango wa Kansela Merkel kuhusu katiba mpya ya Ulaya ni mojawapo ya ufanisi wa sera za nje za Angela Merkel, ambazo zimemfanya kuwa mwanasiasa wa Ujerumani anayependwa zaidi. Hata ufanisi wake ndani ya nchi umemfanya Angela Merkel kuwa maarufu: Ukosefu wa ajira umekuwa ukipungua tangu Merkel alipoingia madarakani kwa takriban nafasi milioni mbili, na mnamo mwaka 2007, kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, Ujerumani ikaongeza fedha za kwa ajili ya bima ya kijamii. Baadaye mgogoro wa kiuchumi ukapiga hodi Ujerumani. Kansela Merkel na serikali yake alianzisha mpango maalum wa kuyaokoa mabenki yasifilisike uliogharimu mabilioni ya euro ukaanzishwa katika awamu ya kwanza na ya pili.

Wanasiasa wa kihafidhina wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, wanamuona vipi kansela Merkel? Waziri mkuu wa jimbo la Baden- Württemburg, Günter Oettinger, anaelezea jinsi wengi katika chama cha CDU wanavyofikiria"Ni kansela wa mseto mkubwa, na ndio maana ninatarajia kutoka kwake kwamba awe kansela anayeweza kufikia makubaliano. Lakini kama mgombea ukansela na mwenyekiti wa chama katika uchaguzi mkuu ujao, anapaswa aonyeshe wazi taswira halisi ya muungano wa CDU na CSU."

Angela Merkel anabakia mwanasiasa mahiri na aliye na msimamo imara. Jambo moja tu linalomtia wasiwasi ni ikiwa wafuasi wake na wapiga kura wa Ujerumani wanaweza kumhakikishia ushindi katika uchaguzi ujao!

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman