1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Binti ya Rais wa Congo ashitakiwa kwa rushwa Ufaransa

Bruce Amani
26 Juni 2017

Uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zinazozihusisha familia tatu za viongozi wa Afrika umefika hadi Ufaransa ambako mali za watuhumiwa nchini humo zinachunguzwa.

https://p.dw.com/p/2fNQO
Kongo Brazzaville Präsidentschaftswahlen Wahllokal Denis Sassou Nguesso
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Duru zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa Julienne Sassou Nguesso, mwenye umri wa miaka 50, na mumewe mwenye umri wa miaka 53 Guy Johnson wamewekwa chini ya uchunguzi wiki hii kwa "kutakatisha pesa na matumizi mabaya ya fedha”.

Wapelelezi wanajaribu kutafuta ni vipi watu hao wawili waliweza kununua jumba kubwa la kifahari mnamo mwaka wa 2006 kwa kiasi cha euro milioni 3 katika kitongoji kimoja cha Paris cha Neuilly-sur-Seine kaskazini kwa mujibu wa duru ya mahakama.

Kesi hiyo inazifikia familia tawala nchini Guinea ya Ikweta na Gabon. Julliene Sassou Nguesso ni wakala wa bima na mumewe ni wakili. Kati ya mwaka wa 2007 na 2011, jumba hilo lenye vyumba saba vya kulala na bwawa la kuogelea la ndani lilifanyiwa ukarabati wa euro milioni 5.34, na kuongeza kiasi cha uwezekezaji wa watu hao wawili kufikia karibu euro milioni 10.

Wapelelezi wanaamini kuwa mwanamke huyo na mumewe huenda walifadhili sehemu ya mradi huo kupitia kampuni ya kigeni nchini Ushelisheli na mauzo ya hisa alizomiliki Julienne Sassou Nguesso katika kampuni moja ya mawasiliano ya simu inayohusishwa na operesheni za ufisadi.

Ali Bongo Ondimba, neuer Präsident von Gabun
Rais Ali Bongo Ondimba wa GabonPicha: AP

Aidha wachunguzi waligundua kuwa mamilioni ya euro ya fedha za serikali yamesafirishwa kutoka Brazzaville tangu mwaka wa 2007 hadi kwenye akaunti za kigeni nchini Ushelisheli, kisiwa cha Mauritius na Hong Kong, ambazo wanamini walizitumia kufadhili maisha ya kifahari ya jamaa za familia ya rais.

Johnson pia yuko chini ya uchunguzi kutokana na jukumu ambalo huenda alitekeleza akiwa msimamizi wa mali katika kampuni moja ya biashara ya majumba ambayo katika mwaka wa 2007 ilinunua jumba kubwa la kifahari kwa thamani ya euro milioni 19 katika eneo jingine la watu wa kipato cha juu mjini Paris.

Binti yake mkubwa Rais Denis Sassou Nguesso, Edith Lucie Bongo Ondimba, ambaye ni mke wa rais wa zamani wa Gabon marehemu Omar Bongo Ondimba aliyefariki dunia 2009, pia alikuwa na hisa katika kampuni hiyo.

Maafisa wa Ufaransa wamekuwa wakiuchunguza ukoo mzima wa Sassou Nguesso pamoja na jamaa za Omar Bongo na mwanawe wa kiume ambaye ni kiongozi wa sasa wa Gabon na Rais Teodoro Obiang Nguema wa Guinea ya Ikweta.

Mwanawe Obiang, Teodorin, kwa sasa anapambana na kesi katika mahakama ya Paris kwa madai ya kupora mali za nchi hiyo ili kufadhili maisha yake ya kifahari.

Äquatorialguinea Teodoro Obiang Nguema Mangue
Teodoro Obiang Nguema anachunguzwa kwa rushwaPicha: Getty Images/AFP/A. Senna

Teodorin mwenye umri wa miaka 48, anaefahamika kwa kupenda magari na majumba ya kifahari na suti za bei ghali, anashukiwa kutumia zaidi ya euro milioni 100 fedha za serikali zilizotokana na ufisadi, kununua jumba kubwa kwenye mtaa wa Avenue Foch, mjini Paris pamoja na magari kadhaa ya kifahari Italia.

 Obiang amekanusha madai hayo akisema fedha hizo zilitokana na vyanzo halali. Kesi hiyo ilitumika kama chanzo cha kesi nyingine za aina hiyo nchini Ufaransa ambayo kwa muda mrefu imewafumbia macho madikteta wa Kiafrika wakiwekeza katika biashara ya majumba na bidhaa za kifahari mapato yao waliyoyapata kwa njia za uovu.

Ilikuja baada ya karibu mwongo mmoja wa shinikizo kutoka kwa makundi ya wanaharakati Sherpa na Transparency. Tayari mwezi Machi, mpwa wa Rais wa Congo Brazzaville, Wilfried Nguesso, aliwekwa chini ya uchunguzi kwa tuhuma sawa na hizo. Matukio hayo ni sehemu ya mfululizo wa uchunguzi unaofanywa na maafisa wa Ufaransa kuhusiana na mali za familia za marais watatu wa kiafrika ambao ulionza mwaka wa 2010.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga