Binti wa rais wa zamani wa Angola anakanusha madai ya ufisadi | Matukio ya Afrika | DW | 01.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Angola

Binti wa rais wa zamani wa Angola anakanusha madai ya ufisadi

Binti wa rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos amekanusha madai ya ufisadi  baada ya mahakama mjini Luanda kuifunga akaunti yake ya benki. Isabel dos Santos amesema madai hayo dhidi yake yamechochewa kisiasa.

Isabel dos Santos anayeaminiwa kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika anachunguzwa kwa madai ya kufanya ubadhirifu wa fedha na kuzisababishia hasara kubwa kampuni za serikali ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa ya mafuta ya taifa  ‘Sonangol‘.

Baba yake Jose Eduardo dos Santos aliitawala Angola kwa miaka 38 na utawala wake unahusishwa na kukithiri kwa ufisadi na ubaguzi  kwa madai kwamba aliyekuwa rais dos Santos aliwapendelea watu wa familia katika kuwapa vyeo serikalini hadi Rais Joao Lourenco alipochukua nafasi yake mnamo mwaka 2017.

Isabel, kama wengi wa wanafamilia ya dos Santos, aliondoka Angola, akidai alikabiliwa na vitisho vya kuuliwa baada ya baba yake kuondoka madarakani.

Aliteuliwa kuwa mkuu wa kampuni ya matuta ya taifa Sonangol mnamo mwaka 2016 lakini alitolewa kwenye wadhfa huo mwaka uliofuata wa 2017, katika hatua ya kwanza iliyofanywa na rais wa Angola Joao Lourenco ya kuwaondoa jamaa za dos Santos kutoka kwenye nyadhifa mbalimbali.

Bildkombo Angola - Joao Manuel Goncalves Lourenco und Jose Eduardo Dos Santos

Kushoto: Rais wa Angola Joao Manuel Goncalves Lourenco. Kulia aliyekuwa Rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos

Mahakama ya Angola, kama sehemu ya upelelezi wake imetoa amri ya kuzifunga akaunti za benki za Isabel dos Santos na mumewe Sindika Dokolo. Taarifa zaidi zinasema kuwa hisa zao katika kampuni kadhaa za Angola, pamoja na kampuni ya simu ya Unitel  na kampuni ya simenti ya Cimangola, pia zimeshikiliwa na mahakama.

Mwana wa rais wa zamani, Jose Filomeno dos Santos, mwenye umri wa miaka 41, ambaye ni kaka wa Isabel dos Santos, mapema mwezi Desemba alifikishwa mahakami kwa tuhuma za ufisadi. Anatuhumiwa kwa kufuja kiasi cha dola bilioni 1.5 kutoka kwenye mfuko wa mali za taifa la Angola wakati wa alipokuwa mkuu wa mfuko huo kuanzia mwaka  2013 hadi mwaka 2018.

Uamuzi wa mahakama hiyo pia unamuhusu mfanyabiashara wa Ureno, Mario da Silva. Familia yake inailaumu serikali ya rais Lourenco kwa misukosuko inayomkabili da Silva.

Darias Jonker, mkurugenzi wa bara la Afrika wa Eurasia Group, kampuni ya ushauri inayohusika pia na utafiti wa masuala ya kisiasa amesema kufungiwa mali za familia ya dos Santos inaonyesha kwamba rais Lourenco anahisi sasa anaweza kusonga mbele dhidi ya familia ya dos Santos katika vita dhidi ya ufisadi bila kuhatarisha ushawishi wake ndani ya chama tawala cha MPLA.

Licha ya utajiri mkubwa wa mafuta, gesi na madini, wananchi wengi wa Angola wanaishi katika umaskini na wanaendelea kutegemea kilimo kwenye mashamba madogo madogo kujikimu mahitaji yao ya msingi.

Vyanzo:RTRE/AFP