Biden, Stoltenberg waujadili mkutano ujao wa NATO | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden, Stoltenberg waujadili mkutano ujao wa NATO

Rais wa Marekani Joe Biden na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wamekubaliana kuwa kuimarisha muungano huo wa kijeshi wa nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini ni muhimu katika wakati huu wa ushindani wa kimataifa

Mkutano wa Biden na Stoltenberg ulihusu maandalizi ya mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa wanachama wa NATO mnamo Juni 14 mjini Brussels ambao Biden atahudhuria kama sehemu ya ziara yake ya kwanza ya kigeni akiwa rais. Akizungumza na waaandishi wa habari nje ya Ikulu ya Marekani baada ya mkutano na Biden, Stoltenberg amesema mkutano wa wiki ijayo wa NATO utatuma ujumbe imara wa umoja wa jumuiya hiyo "NATO yenye nguvu ni nzuri kwa Ulaya, lakini pia ni nzuri kwa Marekani. Hakuna nchi nyingine yenye nguvu iliyo na marafiki wengi na washirika kama ilio nao Marekani katika NATO. Kwa hiyo nasubiri kumkaribisha Rais Biden Brussels. Namsubiri yeye na viongozi wengine wa NATO kwa mkutano wa kilele katika siku tatu zijazo."

Mkuu huyo wa NATO amewahimiza washirika "kuwekeza Zaidi” katika ulinzi wa muungano huo na hicho ndicho wanachokifanya kwa sasa.  Walijadili jinsi ya kuuimarisha muungano huo dhidi ya changamoto zikiwemo ugaidi wa ulimwengu na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na mahusiano yaliyoharibika na Urusi na China.

Belgien COVID-19 | NATO-Hauptquartier in Brüssel

Makao Makuu ya NATO mjini Brussels

Mbinu ya "Barabara ya pande mbili” na Urusi

Stoltenberg amesema amekubaliana na Biden kuhusu mbinu ya "barabara ya pande mbili” ya "kuizuia, ulinzi na mazungumzo” na Urusi.

Soma pia: NATO: Urusi iache kuwapeleka wanajeshi mpakani mwa Ukraine

Katika ziara ya kwanza ya kigeni ya Biden akiwa rais, pia atahudhuria mkutano unaosubiriwa kwa hamu, na Rais wa wa Urusi Vladmir Putin mjini Geneva, baada ya kuhudhuria mikutano ya NATO na wa kundi la mataifa tajiri ulimwenguni – G7 mjini London kuanzia Juni 11 hadi 13.

Mshauri wa Biden kuhusu Usalama wa Taifa Jake Sullivan amesema mkutano wa Biden na Putin utakuja wakati mzuri kwa sababu Biden atakuwa ameshauriana na washirika wake wa Ulaya. Sullivan amesisitiza kuwa Biden hakutani na Putin licha ya tofauti zao, bali kwa sababu ya tofauti zao "Umuhimu wa ziara hiyo ni kukuza sera ya kigeni ya Joe Biden. Kuyamahamisha mataifa ya ulimwengu kupambana na changamoto za wakati huu."

China haishiriki maadili yetu

Stoltenberg amekiri kuwa ushirikiano na China unatoa fursa kwa mataifa ya Magharibi, lakini bado kuna masuala ambayo yanafanya mahusiano kuwa magumu na China. Alilaani sera za kulazimisha za China kuelekea Taiwan, Uighur na waandamanaji wa Hong Kong, lakini akasema washirika wa NATO wanahitaji kujadili na China masuala kama vile mabadiliko ya tabia nchi na udhibiti wa silaha.

dw