1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Putin wakutana Geneva

Saumu Mwasimba
16 Juni 2021

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin wanakutana mjini Geneva kwenye mkutano wao wa kilele.

https://p.dw.com/p/3v2KO
Schweiz Genf | Gipfeltreffen Biden und Putin
Picha: Patrick Semansky/AP/picture alliance

Mkutano kati ya viongozi hao wakuu wa nchi mbili muhimu duniani umetawaliwa na kiwingu cha wasiwasi huko mjini Geneva, ambapo jinamizi la vita vya baridi likiwa bado lipo pembeni, hivi sasa Marekani ina wasiwasi kuhusu mashambulizi ya mtandao yanayofanywa na Urusi na kile ambacho Marekani inakiona kama ni mwelekeo hatari wa kiimla wa nchi hiyo ya Urusi.

Mkutano kati ya Biden na Putin umepangiwa kuchukua muda wa hadi masaa matano kuanzia saa saba mchana na wala hakutokuwa na mapumziko ya kupata chakula. Kwa sababu aliulizwa afisa mmoja mwandamizi wa Marekani ikiwa viongozi hao wawili watakula pamoja kama hatua ya kuonesha ishara ya nia njema katika mkutano huo kuhusu diplomasia, afisa huyo alijibu kwamba hilo halitotokea na hakuna mapumziko ya kula chakula yatakayofanyika.

Soma pia: Urusi yaijibu Marekani kwa kuwatimua wanadiplomasia wake

Joe Biden (Kushoto) na Vladimir Putin (kushoto)
Joe Biden (Kushoto) na Vladimir Putin (kushoto)Picha: Denis Balibouse/Reuters/AP/picture alliance

Mji wa Geneva kuchaguliwa kuwa sehemu ya kufanyika mkutano huu imetokana na mazungumzo marefu baina ya Marekani na Urusi yakikumbushia mkutano wa kilele enzi za vita baridi kati ya marais wakati huo, mnamo mwaka 1985, rais wa Marekani Ronald Reagan na Mikhail Gorbachev aliyekuwa akiongoza umoja wa Kisoviet.

Ulinzi mkali umewekwa katika Jumba la kifakhari unakofanyika mkutano huo eneo la milimani ambapo maboti ya doria yanazunguuka kwenye ziwa lililoko karibu na jengo hilo na wanajeshi wenye silaha wanalinda eneo zima la karibu na hapo.

Soma pia: NATO yaitaka Urusi kuacha kuwapeleka wanajeshi mpakani mwa Ukraine

Katika mkutano huu tofauti na ule wa enzi za vita baridi, sio kuhusu mvutano juu ya silaha za kimkakati za Nuklia na ushindani wa kiitikadi bali ni kile ambacho serikali ya rais Biden inakiona ni kuongezeka uchokozi na uvunjwaji sheria unaofanywa na serikali ya Kremlin.

Usalama waimarishwa Geneva wakati Rais Joe Biden na Vladimir Putin wanakutana
Usalama waimarishwa Geneva wakati Rais Joe Biden na Vladimir Putin wanakutanaPicha: Björn Trotzki/imago images

Kuanzia mashambulizi ya kimtandao dhidi ya taasisi za Marekani na kuingiliwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo hadi ukiukaji wa haki za binadamu na matumizi ya nguvu dhidi ya Ukraine na nchi nyingine za Ulaya na orodha hiyo ya malalamiko ya marekani dhidi ya Urusi ni ndefu.

Hata hivyo rais Putin ana hoji kwamba inachokitaka Moscow ni kitu rahisi na kuupinga ubabe wa nchi moja Marekani wa kutaka kuitawala dunia. Hoja hiyo ya Urusi ni sehemu ya kutafuta kuunga mkono kile kinachoitwa usawa katika uongozi wa dunia, suala ambalo Urusi na China zinalipigia upatu.