1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Putin kujadiliana matakwa ya Urusi kuhusu usalama

30 Desemba 2021

Marais Joe Biden wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi watazungumza kwa njia ya simu leo katika wakati Moscow imechachamaa kutafuta uhakika kwamba usalama wake hautawekwa rehani kupitia ardhi ya mashariki mwa Ulaya.

https://p.dw.com/p/44yMZ
Schweiz l Biden und Putin treffen sich in Genf l Begrüßung
Picha: Patrick Semansky/AP/picture alliance

Kulingana na msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa nchini Marekani Emily Horne, viongozi hao wawili watajadili masuala kadhaa ikiwemo mashauriano ya ngazi ya juu kati ya Marekani na Urusi yaliyopangwa kufanyika mjini Geneva mwanzoni mwaka unaokuja.

Mazungumzo ya leo kati ya Biden na Putin yatafanyika wakati Marekani na washirika wake wa magharibi wameshuhudia Urusi ikiendelea kulundika mamia kwa maelfu ya wanajeshi wake karibu na mpaka na Ukraine hali inayozidisha wasiwasi kuwa Kremlin ina mipango ya kuivamia nchi hiyo.

Katika mkutano wa leo ambao uliombwa na Urusi, Biden anatarajiwa kumweleza kwa mara nyingine na bila kificho Bw. Putin kwamba Washington inasimama imara na kwa mshikamano na washirika wake wa magharibi lakini itakuwa tayari kufanya mazungumzo na Urusi chini ya diplomasia ya kuheshimiana.

Marekani yasema mshikamano wake na mataifa ya Ulaya ni imara 

Ikulu ya Marekani imesema iliridhia kuandaa mazungumzo ya leo kwa sababu inaamini mashauriano kati ya wakuu wa nchi ni muhimu hasa nyakati hizi ambazo kitisho cha Urusi kuivamia Ukraine kimezusha hamkani kubwa barani Ulaya.

Russland Yelnya | Satellitenbild | Russisches Militär
Vikosi vya Urusi karibu na mpaka wake na Ukraine Picha: Maxar Technologies/AFP

Yumkini mataifa ya Ulaya yana kumbukumbu ya mwaka 2014 wakati vikosi vya Urusi vilipoosonga mbele na kuimakata rasi ya Crimea iliyo kwenye bahari nyeusi kutoka himaya ya Ukraine na hapakuwa na chochote cha kufanya kuikabili Moscow.

Hapo jana waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken alizungumza na rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine kumhakikishia kwamba utawala mjini Washington hauitatupa mkono Kiev mbele ya ubabe wa Urusi.

Je, mazungumzo ya leo yatazaa matunda? 

Sotschi, Russland |Putin in Videokonferenz mit Biden
Rais Vladimir Putin wa Urusi alipozungumza kwa mara ya mwisho na mwenzake wa Marekani Joe Biden mwanzoni mwa mwezi DisembaPicha: Mikhail Metzel/dpa/picture alliance

Urusi yenyewe ndiyo inalalamika ikisema haitakuwa na chaguo isipokuwa kulinda maslahi yake iwapo mataifa ya magharibi hayatatimiza matwaka yake ya kutoikaribisha Ukraine kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami, NATO.

Kwa ikulu ya Kremlin na rais Putin kuvisogeza vikosi vya NATO karibu kabisa na mipaka ya Urusi mfano wa nchini Ukraine itakuwa mstari mwekundu ambao katu haupaswi kuvukwa.

Urusi ilikwishawasilisha mapema mwezi huu mkururo wa matakwa yake ikiirai Jumuiya ya NATO kutoikaribisha Ukraine na madola mengine ya uliokuwa muungano wa kisovieti na pia ipunguze idadi ya wanajeshi na vifaa inavyipeleka katika mataifa ya  Ulaya kati na mashariki.

Hata hivyo Marekani na washirika wake walikataa kuipatia Urusi hakikisho lolote wakisema kwa misingi ya  NATO uanachama uko wazi kwa taifa lolote linalokidhi vigezo. Kutokana na mivutano hiyo, Marekani na Urusi zikakubaliana kwamba zikutane  Januari 10 kujadili tofauti zilizopo na kutafuta majibu mujarabu.

Lakini kwa kuanzia itakuwa ni mkutano wa leo kati ya vigogo wawili yaan Biden na Putin na wengi wanasubiri kuona iwapo yatakuwa mazungumzo ya manufaa au yatasadifu ile methali ya kiswahili ya kila mwamba ngoma huvuta upande wake.