Biden: Marekani kuiunga mkono Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden: Marekani kuiunga mkono Ukraine

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ameahidi kuwa nchi yake itaisaidia Ukraine kisiasa na kiuchumi pamoja na kuiunga mkono dhidi ya vitisho vya kudhalilisha, na ameonya kuwa Ukraine inapaswa kupambana na rushwa.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden

Akizungumza mjini Kiev na viongozi wa serikali mpya ya Ukraine inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi, Biden amesema anawasilisha ujumbe wa Rais Barack Obama kwamba Marekani inaiunga mkono serikali ya Ukraine, wakati ambapo Marekani na Urusi zinatupiana lawama kutokana na kukiukwa kwa makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa mjini Geneva wiki iliyopita ya kupunguza mzozo unaoendelea mashariki mwa Ukraine.

Biden amesema Marekani inataka kuwa mshirika na rafiki wa Ukraine wakati huu wa fursa ya kihistoria kwa nchi hiyo kufanya mageuzi ya kisiasa. Amesema uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Mei 25 mwaka huu, utakuwa muhimu katika historia ya Ukraine. Biden amesema kipaumbele cha Marekani ni kuisaidia Ukraine kuwa taifa linalojitegemea na kutoendelea kutegemea usambazaji wa nishati kutoka Urusi.

Biden aionya Ukraine kuhusu rushwa

Akizungumzia suala la rushwa, Biden amesema Ukraine inapaswa kupambana na saratani ya rushwa, inayodhoofisha mfumo mzima kwa sasa. Amesema nchi hiyo inapaswa kuubadilisha mfumo wa mahakama na kutafuta njia sawa za madaraka kati ya rais na bunge la Ukraine linalojulikana kama Rada.

Joe Biden akiwa na Rais Oleksander Turchynov

Joe Biden akiwa na Rais Oleksandr Turchynov

Kabla ya kukutana na wanasiasa hao, Biden alikutana na Rais wa mpito wa Ukraine, Oleksandr Turchynov katika jengo la bunge, ambapo walizungumzia namna ya kuyatekeleza makubaliano yaliyofikiwa Geneva, ya kupunguza mzozo wa mashariki mwa Ukraine, ambao ni mbaya kabisa kuwahi kutokea tangu enzi za Vita Baridi.

Kulingana na makubaliano hayo yaliyosainiwa kati ya Ukraine, Urusi, Marekani na Umoja wa Ulaya, waasi wanaoiunga mkono Urusi, ambao wanaidhibiti miji kadhaa ya mshariki mwa Ukraine, wanatakiwa kuweka chini silaha na kuondoka katika majengo ya serikali ambayo wanayakalia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry ameitaka Urusi, kuwashinikiza waasi hao kuondoka kwenye majengo hayo. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov ameitaka Marekani kuishawishi serikali ya Ukraine, ambayo Urusi inaishutumu kwa kukiuka makubaliano ya Geneva.

Aidha, Joe Biden amepangiwa pia kukutana na Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk pamoja na wanaharakati wa demokorasia.

Wakati huo huo, Urusi imemzuia kiongozi wa jamii ya Tatar inayoiunga mkono serikali ya Ukraine, kuingia Crimea kwa miaka mitano. Kiongozi huyo, Mustafa Dzhemilev, amepewa taarifa rasmi inayomzuia kurejea Crimea baada ya jimbo hilo kujiunga na Urusi, mwezi uliopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com