1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kusaini maagizo ya kiutendaji baada ya kuapishwa

Grace Kabogo
17 Januari 2021

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden atasaini maagizo kadhaa ya kiutendaji siku ya kwanza baada ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3o1kx
Designierter US-Präsident Biden
Picha: Matt Slocum/dpa/AP/picture alliance

Msaidizi wa ngazi ya juu wa Biden, Ron Klain amesema kwamba maagizo ya kiutendaji yatahusu janga la virusi vya corona, uchumi wa Marekani unaodorora, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ubaguzi wa rangi. ''Majanga yote haya yanahitaji kushughulikiwa haraka,'' alisema Klain ambaye ni mkuu wa watumishi ajaye wa Biden.

Kwa mujibu wa Klain, katika siku zake 10 za kwanza madarakani, Biden atachukua hatua madhubuti kushughulikia mizozo hiyo minne, kuzuia madhara mengine ya haraka na yasiyoweza kurekebishwa pamoja na kuirudisha nafasi ya Marekani ulimwenguni.

Marekani ina takriban watu 400,000 waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 na nchi hiyo inarekodi zaidi ya visa vipya milioni moja kwa wiki, wakati ambapo virusi hivyo vinazidi kuenea. Wiki hii Biden aliuzindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9 kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya corona na kuufufua uchumi.

Soma zaidi: Biden azindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9

Klain amesema siku ya kuapishwa Biden, kama alivyoahidi atasaini maagizo ya rais ikiwemo ya Marekani kujiunga tena kwenye Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi na kuibadili marufuku ya kuwazuia watu kutoka kwenye nchi kadhaa zenye waumini wengi wa Kiislamu kuingia Marekani, ambayo iliwekwa na Rais Donald Trump.

Ronald Klain
Ronald Klain, msaidizi wa ngazi ya juu wa BidenPicha: Nicholas Kamm/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, wafuasi wa Trump wanatarajia kuandamana mjini Washington DC na kwenye majengo ya bunge ya majimbo kuanzia siku ya Jumapili hadi siku ya Jumatano wakati ambapo Biden ataapishwa kuwa rais wa Marekani. Polisi wa majimbo wameimarisha ulinzi mwishoni mwa wiki hii kabla ya Biden mwanachama wa Democratic hajaapishwa Januari 20 na kutokana na wasiwasi wa uwezekano wa kufanyika maandamano ya watu wenye silaha siku ya Jumapili.

Polisi wanajipanga kuzuia kujirudia tena kwa vurugu zilizosababisha vifo baada ya wafuasi wa Trump kuyavamia majengo ya bunge mjini Washington Januari 6. Huku Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI likionya kuhusu uwezekano wa kutokea vurugu kwenye majengo ya bunge ya majimbo, magavana wa Marekani wametangaza hali ya tahadhari na kuyafunga majengo ya bunge kwa umma.

Maandamano yanatarajiwa kufanyika wapi?

Maandamano yanayomuunga mkono Trump huenda yakafanyika kwenye majengo ya bunge ya majimbo yote kuanzia siku ya Jumapili. Ulinzi unaweza kuimarishwa wiki nzima kuanzia Atlanta, Georgia hadi Sacramento, California. Lengo kuu la maandamano linaweza likawa kwenye mji mkuu wa Marekani, Washington ambako Biden ataapishwa kuwa rais wa 46 wa nchi hiyo siku ya Jumatano.

USA I Washington I Kapitol
Askari wakiwa nje ya jengo la bunge la Marekani, WashingtonPicha: Eric Thayer/Getty Images

Maelfu ya askari wa ulinzi wa Marekani wamepelekwa Washington, huku vikosi vya uslama vikiifunga mitaa ya jiji hilo kwa kuweka vizuizi vya zege. Zaidi ya walinzi 25,000 wanatarajiwa kupelekwa kwenye mji huo ifikapo mwanzoni mwa wiki ijayo.

Taarifa za kijasusi zinaeleza kuwa watu wenye silaha huenda wakajaribu kuweka vilipuzi. Siku ya Jumamosi maafisa wa usalama walimkamata mwanaume mmoja mjini Washington akiwa na silaha katika eneo la ukaguzi karibu na jengo la bunge la Marekani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, mwanaume huyo mkaazi wa Virginia alishikiliwa baada ya polisi kumkuta na bunduki, zaidi ya risasi 500 pamoja na maganda ya risasi.

Nini cha kutarajiwa siku ya kuapishwa

Joe Biden ataapishwa kuwa rais wa Marekani na Kamala Harris ataapishwa kuwa makamu wa rais katika sherehe zitakazofanyika mbele ya jengo la bunge la Marekani siku ya Jumatano. Maafisa wameamua kupunguza idadi ya watu wa kuhudhuria sherehe hizo kutokana na janga la virusi vya corona na wasiwasi wa usalama.

USA Wilmington | Rede Joe Biden und Kamala Harris nach dem Wahlsieg
Kamala Harris na Joe BidenPicha: Andrew Harnik/Getty Images

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, Biden, Harris na wenza wao pamoja na marais wa zamani wa nchi hiyo, Barack Obama, George W. Bush, Bill Clinton na wake zao wataweka shada la maua katika kaburi la mwanajeshi asiyejulikana kwenye makaburi ya kitaifa yaliyoko kwenye bustani ya Arlington.

Baada ya hapo, Biden atasindikizwa kwa msafara wa rais kutoka mtaa wa 15 mjini Washington hadi katika Ikulu ya Marekani, White House. Badala ya kuwepo kwa gwaride maalum la kawaida la kijeshi la kuapishwa rais, waandalizi wa sherehe hizo wamepanga kuandaa gwaride litakalotizamwa nchi nzima kupitia televisheni.

(AP, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/2LvqvPP)