1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCambodia

Biden kukutana na Xi Jinping

Saumu Mwasimba
12 Novemba 2022

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuitia msukumo China kuingilia katika suala la Korea Kaskazini,watakapokutana huko Bali Indonesia Jumatatu

https://p.dw.com/p/4JQtI
Kambodia | 2022 ASEAN Gipfeltreffen in Phnom Penh - Joe Biden
Picha: KEVIN LAMARQUE/REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden yuko Cambodia alikowasili leo Jumamosi katika ziara yake barani Asia na ameahidi kumtolea mwito rais wa China Xi Jinping kuingilia kati suala la Korea Kaskazini, watakapokutana ana kwa ana katika kikao watakachokaa wiki ijayo huko Bali.

Katika ziara yake hii ya Cambodia rais Biden amekutana na viongozi wa jumuiya ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia-ASEAN katika mji mkuu Phnom-Penh.

Kambodscha | Ankunft von Joe Biden in Phnom Penh zum ASEAN-Gipfel
Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Hata hivyo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wamemtolea mwito rais wa Marekani Joe Biden alizungumzie suala la kuandamwa jamii ya wachache ya Waiguru huko Kaskazini Magharibi mwa China,atakapokutana na mwenzake wa China Xi Jinping.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana Jumatatu katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia kabla ya mkutano wa kilele wa kundi la G20 utakaofanyika Jumanne.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch tawi la China Sophie Richardson, amesema rais Biden anapaswa kutilia mkazo kwamba nchi yake imejitolea katika  uchunguzi wa kimataifa kuhusu kufuatilia ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya China.

Mkutano kati ya rais Biden na mwenzake Xi utakuwa ni wa kwanza baina yao tangu Biden alipotwaa madaraka nchini Marekani. Shirika la Human Rights Watch linasema maamlaka za serikali ya China zinawaandama watu wa jamii za wachache za waislamu ikiwemo Waiguru na jamii ya Turkic kwa kuwakamata mamilioni yao kutokana na tamaduni zao na kuwashikilia kinyume cha sheria katika vituo maalum huko kwenye jimbo la Xinjiang,ambalo zamani likiitwa Turkestan ya Mashariki.

Kambodia | 2022 ASEAN Gipfeltreffen in Phnom Penh - Joe Biden
Picha: CINDY LIU/REUTERS

Lakini utawala wa China unadai kwamba jamii ya Waiguru inaendesha harakati za kujitenga eneo hilo,itikadi kali pamoja na ugaidi wakati jamii hiyo ya wachache ya waislamu ikihisi kukandamizwa kisiasa,kidini na kitamaduni.

Ikumbukwe kwamba serikali ya Kikomunisti ya China ililiijumuisha eneo hilo katika Jamhuri ya umma wa watu wa China baada ya kuingia madarakani mwaka 1949,wengi katika mkoa huo bado hawalitaki jina la Xinjiang ambalo ni la lugha ya Kimandarin.

 Miito ya watetezi wa haki za binadamu inatolewa wakati viongozi wa serikali kutoka kundi la nchi tajiri na zinazoinukia kiviwanda la G20 wakijiandaa kukutana Jumanne kisiwani Bali nchini Indonesia na mkutano huo utamalizika tarehe 16 Novemba.

Beziehungen Indonesien Europäische Union | Außenministerin Marsudi und Borrell
Picha: Stefani Reynolds/AFP/AP/picture alliance

Mkutano huo utakuwa wa kwanza wa viongozi wa G20 tangu Urusi ilipovamia Ukraine katika kile ambacho Urusi inakiita ni operesheni maalum ya kijeshi,na suala hilo linategemewa kuwa ajenda kuu ya mkutano.

Rais Vladmir Putin hatokwenda kwenye mkutano huo bali atawakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov.Mpaka sasa Indonesia imekataa kutii mashinikizo ya nchi za magharibi ya kuitaka ifute mualiko wa Putin na kuitimua Urusi kwenye kundi hilo kutokana na vita vyake Ukraine,Indonesia inasema haina mamlaka ya kufanya hivyo bila ya maafikiano ya pamoja ya nchi wanachama.