1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kukutana na wataalamu wa COVID-19

Lilian Mtono
9 Novemba 2020

Rais mteule wa Marekani Joe Biden hii anatarajiwa kukutana na kikosi kazi kitakachotathmini janga la corona ambalo ni changamoto ya kwanza kabisa anayokabiliwa nayo mara baada ya kuchukua madaraka Januari mwakani.

https://p.dw.com/p/3l3iq
Joe Biden USA Porträt
Picha: Tasos Katopodis/Getty Images

Rais mteule wa Marekani Joe Biden hii leo anatarajiwa kukutana na kikosi kazi kitakachotathmini janga la virusi vya corona, ambalo ni changamoto ya kwanza kabisa anayokabiliwa nayo mara baada ya kuchukua madaraka Januari mwakani huku rais Donald Trump akiendelea kupambana ili kuhakikisha anasalia kwenye kiti hicho. 

Biden anatarajiwa kukutana na bodi ya ushauri inayosimamiwa na Jenerali Vivek Murthy ambaye ni mtaalamu wa zamani wa upasuaji, kamishna wa zamani wa mamlaka ya chakula na dawa David Kessler na Profesa wa chuo kikuu cha Yale Marcella Nunez-Smith ili kuchunguza namna bora kabisa ya kukabiliana na janga hilo lililosababisha vifo vya zaidi ya Wamerekani 270,000.

Makamu huyo wa zamani wa Rais kutoka  Chama cha Democratic, baada ya hapo atatoa hotuba huko Wilmington, Delaware kuhusiana na mipango yake ya kukabiliana na COVID-19 na kujenga upya uchumi wa taifa hilo.

Soma Zaidi: Uhalisia wasambaratisha uongo wa Trump kuhusu corona

Jopo la Biden pia linamuhusisha mfichuzi Rick Bright anayesema alitimuliwa kutoka kwenye serikali ya Trump baada ya kuelezea wasiwasi kuhusiana na maandalizi ya kukabiliana na janga la covid-19  pamoja na Luciana Borio aliyebobea kwenye dharura ya afya ya umma.

Tedros Adhanom Ghebreyesus, Direktor WHO
Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameahidi kushirikiana kwa karibu na Marekani katika kuliimarisha shirika la WHOPicha: Reuters/D. Balibouse

Wakati Biden akitarajiwa kukutana na kikosi kazi hicho, mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amekaribisha juhudi za kuliimarisha shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva na kusema anatarajia kufanya kazi kwa karibu na serikali ya rais mteule wa Marekani Joe Biden.

"Tunampongeza rais mteule Joe Biden na makamu wa rais mteule Kamala Harris na tunatarajia kufanya kazi na utawala huu kwa karibu sana. Tunahitaji kufikiria upya uongozi uliojengwa kwenye misingi ya kuaminiana na uwajibikaji wa pande zote ili kumaliza janga hilo." alisema Tedros.

Gebreyesus aliyeko karantiki amewaambia mawaziri wa afya kwa njia ya video wakati wa mkutano wa mwaka kwamba bado kuna mengi ya kufanya ingawa wanaamini kwamba wapo kwenye mstari. Marekani chini ya Trump ilisitisha ufadhili kwa shirika hilo na kuanza mchakato wa kujiondoa hatua iliyobua ukosoaji mpana katikati ya mzozo wa COVID-19.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Ulaya umesema utasubiri kwanza rais huyo mteule, Joe Biden aingie madarakani kabla ya kutoa kauli yake kuhusiana na mustakabali wa kimahusiano na Washington. Msemaji wa umoja huo wa mataifa 27 Eric Mamer ameuambia mkutano wa wanahabri kwamba wamesikia kuhusu mchakato unaoendelea nchini humo na ni mapema bado kutamka chochote hadi pale atakapochukua rasmi madaraka.

Mashirika: DPAE/RTRE