Biden kuhudhuria mkutano wa kilele wa ASEAN | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden kuhudhuria mkutano wa kilele wa ASEAN

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang kuhudhuria mkutano wa kilele wa kila mwaka wa ushirikiano kati ya mataifa ya Asia na Marekani kwa njia ya video.

Mkutano huo unajiri katika ukanda ambao mataifa yenye nguvu yamekuwa yakipigana kumbo kuhusu biashara, uhuru wa Taiwan, demokrasia, haki za binadamu na kuongezeka kwa visa vya uchokozi. 

Rais wa Urusi Vladimir Putin pia anatarajiwa kuuhutubia mkutano huo wa kilele wa siku tatu unaofanyika Brunei chini ya uandalizi wa mataifa kumi wanachama wa Jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa bara Asia, ASEAN. Masuala kadhaa wa kadha yanatarajiwa kujadiliwa kuanzia siasa, usalama, demokrasia na uchumi.

Shirika la Afya Duniani WHO linatarajiwa kuwaarifu viongozi kuhusu hali ya janga la Covid-19 ambalo limerudisha nyuma chumi za nchi 18 zinazowakilisha zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu ulimwenguni na huchangia zaidi ya asilimia 60 ya pato jumla la ulimwengu.

Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani imesema Rais Biden atasisitiza uungwaji wake mkono muungano huo wa ASEAN na kujadili dira yake ya kufanya kazi pamoja na washirika hao katika kukabili masuala yanayokumba kanda ya Indo-Pasific.

Marekani kuhudhuria mkutano wa ASEAN baada ya kipindi kirefu cha kutohudhuria

Rais wa Marekani hajahudhuria kikao chochote cha nchi wanachama wa ASEAN tangu mwaka 2017 wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Rais wa Marekani hajahudhuria kikao chochote cha nchi wanachama wa ASEAN tangu mwaka 2017 wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Hii itakuwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017 kwa rais wa Marekani kuhudhuria mkutano wa muungano wa kilele wa ASEAN.

Soma: Blinken aitaka ASEAN kuishinikiza Myanmar kukomesha vurugu

Katika mkutano mwingine na viongozi wengine wa ASEAN jana Jumanne, Rais Biden alitangaza mpango wa dola milioni 100 kuimarisha ushirikiano wa Marekani na kanda hiyo, mnamo wakati China imeendelea kukua kama adui kiusalama na pia kiuchumi.

Fedha hizo zitafadhili miradi ya afya, elimu, uchumi na mipango mipya ya vita dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi miongoni mwa nchi wanachama.

Mahusiano kati ya Marekani na China yamedorora tangu kipindi cha utawala wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump. Wakati huo nchi hizo zilishinda zikikabiliana kibiashara, kidiplomasia miongoni mwa masuala mengine.

Mvutano wa China na Taiwan watarajiwa kujadiliwa

Masuala kadhaa yanatarajiwa kujadiliwa kuanzia siasa, usalama, demokrasia na uchumi.

Masuala kadhaa yanatarajiwa kujadiliwa kuanzia siasa, usalama, demokrasia na uchumi.

Huku kukiwa na mvutano unaoendelea kati ya China na Taiwan, hivi karibuni Biden alisema Marekani iko tayari kuisaidia Taiwan iliyo na mamlaka yake ya ndani, lakini ambayo China inadai ni sehemu ya milki yake. Biden alisema Marekani itaisaidia Taiwan kujilinda endapo itashambuliwa.

Mkataba wa Uingereza na Australia kuhusu nyambizi ambao umeighadhabisha China pia huenda pia ukaibuliwa katika mkutano wa pembezoni leo na kiongozi wa Australia.

Baadhi ya nchi za ASEAN, mathalan Indonesia na Malaysia zinahofia mkataba huo unaweza kuzidisha mvutano katika maeneo tete kama vile bahari ya kusini mwa China.

Soma: ASEAN na washirika wengine wasaini mkataba wa kibiashara

Akiuhutubia mkutano huo, Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison, amesema nchi yake itatoa dozi milioni 10 za chanjo ya Covid-19 pamoja na msaada wa dola milioni 92.6 kwa ukanda wa kusini mashariki mwa Asia, mnamo wakati nchi yake inaimarisha ushirikiano na ukanda huo.

Morrison alitilia mkazo umuhimu pendekezo la mkakati kabambe wa ushirikiano na mataifa kumi wanachama wa jumuiya hiyo.

(APE, RTRE)