Biden: Haki imepatikana, lakini haitoshi | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden: Haki imepatikana, lakini haitoshi

Rais wa Marekani, Joe Biden amesema kutiwa hatiani kwa askari polisi aliyemuua George Floyd ni hatua moja kubwa kuelekea katika njia ya kupatikana haki nchini Marekani.

Akizungumza jana katika Ikulu ya Marekani muda mfupi baada ya majaji wa mahakama ya Minneapolis kumtia hatiani Derek Chauvin kwa mashtaka yote matatu ya mauaji, Biden hata hivyo ameonya kuwa Marekani haipaswi kutosheka na hukumu hiyo.

Biden ambaye alizungumza akiwa na makamu wake, Kamala Harris, amesema uamuzi kama huo ni nadra sana kutolewa nchini Marekani.

Weltspiegel 15.04.2021 | USA Washington | Präsident Joe Biden zu Truppenabzug Afghanistan

Rais Joe Biden wa Marekani

Biden amesema hawatoishia hapo na kinachotakiwa sasa ni kusonga mbele hadi mfumo mzima wa ubaguzi wa rangi utakapobadilishwa. Akizungumza na familia ya Floyd baada ya uamuzi wa majaji kutangazwa, Rais Biden alisikika akisema angalau kwa sasa kuna haki.

''Mauaji ya George Floyd yalisababisha maandamano ambayo hatujawahi kushuhudia tangu enzi za kutetea haki za raia katika miaka ya 60, maandamano yaliyowaunganisha watu wa kila rangi na kila kizazi kwa amani na kwa malengo.

Nimezungumza pia na familia ya George Floyd, yenye ujasiri mkubwa. Hakuna kitakachoweza kumrudisha ndugu yao. Lakini hii inaweza kuwa hatua kubwa katika vita dhidi ya ubaguzi na uamuzi mzuri wa kupata haki nchini Marekani,'' alifafanua Biden.

Hukumu kamili kutolewa ndani ya miezi miwili

Chauvin askari polisi wa zamani Mweupe amekutwa na hatia ya kumuua Floyd Mmarekani Mweusi na majaji wamesema hukumu yake inatarajiwa kutolewa ndani ya kipindi cha miezi miwili na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 40 gerezani.

USA Reaktionen Urteil Floyd-Prozess

Wengi wamepokea uamuzi dhidi ya Chauvin kwa furaha

Uamuzi huo umetolewa baada ya wiki tatu za kutoa ushahidi. Majaji walijadiliana chini ya saa 11 kabla ya kumtia hatiani Chauvin kwa mashtaka yote matatu ya mauaji yaliyokuwa yanamkabili.

Baada ya kukutwa na hatia Chauvin, mwenye umri wa miaka 45 alifungwa pingu na kurejeshwa rumande. Hata hivyo, anatarajiwa kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Uamuzi huo ulipokelewa kwa shangwe kubwa na maelfu ya watu nchini Marekani. Takriban watu 300 walikusanyika karibu na uwanja wa mahakama ya Minneapolis kusikiliza uamuzi wa majaji katika kesi hiyo. Baada ya uamuzi kutolewa wengi walikumbatiana, huku wengine wakibubujikwa na machozi.

Uamuzi huo umepongezwa pia na viongozi wengine wa kisiasa na kiraia pamoja na watu maarufu nchini Marekani.

Miongoni mwao ni rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, Oprah Winfrey na Gavana wa California, Gavin Newson, Mmarekani Mweupe na ambaye katika ukurasa wake wa Twitter aliandika kuwa Floyd angekuwa hai hadi leo kama angefanana na yeye, akimaanisha kuwa angekuwa Mmarekani Mweupe basi asingeuawa.