Biden atangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa kijeshi Myanmar | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden atangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa kijeshi Myanmar

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuidhinisha amri ya kiutendaji ya kuwawekea vikwazo vipya wahusika wa mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar na kusisistiza kurejeshwa demokrasia na kuwaachia viongozi wa kiraia. 

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuidhinisha amri ya kiutendaji ya kuwawekea vikwazo vipya waliohusika na mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar na kurejelea wito wake wa kurejeshwa demokrasia pamoja na kuwaachia viongozi wa kiraia. 

Biden amesema amri hiyo itawezesha utawala wake "kuwawekea vikwazo haraka viongozi wa kijeshiambao walihusika na mapinduzi, maslahi yao ya kibiashara sambamba na jamaa zao wa karibu". Rais Biden ameongeza kuwa wiki hii Marekani itabainisha awamu ya kwanza ya wale wataoguswa na vikwazo hivyo na vilevile inawazuia majenerali nchini Myanmar kuweza kuzifikia mali zenye thamani ya dola bilioni 1 katika fedha za serikali ya Myanmar zilizoko Marekani.

"Wakati maandamano yakiongezeka, unyanyasaji dhidi ya wale wanaodai haki zao za kidemokrasia haukubaliki na tutaendelea kuupinga. Watu wa Burma wanapaza sauti zao, na ulimwengu unaangalia. Tutakuwa tayari kuweka hatua za ziada na tutaendelea kushirikiana na washirika wetu wa kimataifa kuhimiza mataifa mengine yajiunge nasi katika juhudi hizi. "

Mapinduzi ya kijeshi ya Februari mosi ambayo yalimuondoa mamlakani kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia Aung San Suu Kyi, yalitokea chini ya wiki mbili baada ya Biden kuapishwa na kuonekana kuwa mtihani wa mapema kwa kiongozi katika kushughulikia migogoro ya kimataifa.

Myanmar Proteste | Ausgangssperre und Versammlungsverbote

Maelfu ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi

Nchi za magharibi zimelaani mapinduzi hayo, lakini wachambuzi wanasema kwamba jeshi la Myanmar halitoweza kutengwa kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, wakati kukiwa na uwezekano mkubwa wa China, India na mataifa jirani ya Kusini mwa Asia na Japan kutokata mahusiano na taifa hilo kutokana na umuhimu wake.

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kesho litakubaliana juu ya azimio lililoandaliwa na Uingereza na Umoja wa Ulaya katika kulaani mapinduzi hayo. Hata hivyo wanadiplomasia wanasema China na Urusi ambazo zote zina mahusiano na vikosi vya Myanmar huenda vikaleta upinzani wa azimio hilo.  Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameonya kwamba muungano huo unaweza kuliwekea vikwazo vipya jeshi la nchi hiyo, lakini hatua hizo zitachukuliwa kwa umakini ili zisiwaathiri wananchi.

Wakati huohuo waandamanaji wamerejea kwenye mitaa ya miji mikubwa licha ya mwanamke mmoja kupigwa risasi siku moja iliyopita. Wanasiasa zaidi wa chama cha kiongozi aliyeondolewa mamlakani Aung San Suu Kyi, wamekamatwa wakiwemo pia waandishi wa habari wakati wa maandamano yanayoendelea. Ingawa Biden hakuweka wazi akina nani hasa watalengwa na vikwazo vipya lakini kiongozi wa mapinduzi Min Aung Hlaing na majenerali wengine ambao tayari wamo kwenye vikwazo vya Marekani vya mwaka 2019 juu ya ukandamizaji wa waislamu wa jamii ya Rohingya huenda watakuwamo katika orodha mpya.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com