Biden atangaza shehena mpya ya silaha kuisaidia Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.05.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden atangaza shehena mpya ya silaha kuisaidia Ukraine

Rais Joe Biden ametangaza shehena mpya ya silaha za Marekani yenye thamani ya dola milioni 150 kwa ajili ya kuisaidia Ukraine kupambana na Urusi.

Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Marekani, shehena hiyo inajumuisha risasi 25,000, rada za kutambua sehemu zilipo silaha za adui pamoja na vipuri. Kabla ya tangazo hilo la jana Ijumaa, utawala wa rais Biden tayari ulikuwa umeshatuma shehena nyengine ya silaha zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3.4 kwa Ukraine.

Shehena hiyo mpya inamaanisha kuwa kiasi dola milioni 250 zilizoidhinishwa awali ili kuisadia Ukraine zimekwisha. Biden analishinikiza bunge la Marekani kuidhinisha msaada mwengine wa dola bilioni 33 kuisaidia Ukraine, ikiwemo dola bilioni 20 za usaidizi wa kijeshi.

Soma pia: Amnesty: Urusi imefanya uhalifu wa kivita, Ukraine

Rais huyo wa Marekani na viongozi wengine wa kundi la mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani G7 pamoja na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, wanatarajiwa kufanya mkutano kwa njia ya mtandao kesho Jumapili kujadili uungwaji mkono wa nchi za Magharibi katika mapambano yao dhidi ya Urusi.

Biden amesema katika taarifa "Marekani imetoa kiasi kikubwa cha fedha ili kuisaidia Ukraine haraka iwezekanavyo. Tunatuma silaha na vifaa vyengine muhimu ambavyo bunge la Congress lilikuwa limeidhinisha."

Rais huyo wa Marekani hata hivyo amesema ufadhili huo unakaribia kuisha, na kwamba iwapo Ukraine itakuwa na fursa yoyote ya kufanikiwa katika vita vyake dhidi ya Urusi, basi Marekani na washirika wake wanapaswa kuipiga jeki Ukraine kwa kuipelekea silaha.

Watu zaidi waokolewa kutoka mji wa bandari wa Mariupol

Ukraine | Evakuierte aus dem Azovstal Stahlwerk

Raia wa Ukraine wakiokolewa kutoka kiwanda cha chuma cha Azovstal

Makumi ya watu wameokolewa kutoka kiwanda cha chuma kilichozingirwa ambapo wapiganaji wa Ukraine mjini Mariupol wamekuwa wakipambana kuzuia vikosi vya Urusi kuchukua udhibiti kamili wa mji huo muhimu wa kimkakati uliokuwa ngome yao ya mwisho.

Maafisa wa Urusi na Ukraine wamesema watu 50 wameokolewa kutoka kiwanda cha chuma cha Azovstal na kukabidhiwa kwa wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu. Jeshi la Urusi limesema, 11 kati ya waliookolewa ni watoto.

Soma pia:Umoja wa Ulaya wataka kupiga marufuku mafuta ya Urusi

Maafisa wa Urusi na Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk wamesema zoezi la uokoaji litaendelea tena leo Jumamosi. Watu hao waliookolewa wanajumuisha wengine wapatao 500 waliokolewa kutoka mji wa Mariupol katika siku za hivi karibuni.

Kulingana na makisio ya Urusi, takriban wapiganaji 2,000 wa Ukraine, wamejificha kwenye mashimo ya chini kwa chini karibu na kiwanda cha chuma cha Azovstal, na kwamba wamekataa miito ya kujisalimisha.

Tazama vidio 02:05

Shinikizo laongezeka kwa Ujerumani kutuma silaha nzito Ukraine

Maafisa wa Ukraine wamesema kabla ya zoezi la siku ya Ijumaa la kuwaokoa mamia ya raia waliokwama huko, wasiwasi juu ya usalama wao unazidi kuongezeka wakati vita vikipamba moto.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa hawajasema lolote juu ya zoezi hilo la uokoaji japo inaaminika kwamba raia waliookolewa watahamishwa hadi Zaporizhzhia, mji unaodhibitiwa na Ukraine karibu kilomita 230 kaskazini magharibi mwa Mariupol.

Baadhi ya manusura waliozungumza na shirika la habari la Associated Press, wameelezea hali ya kutisha kwenye mashimo walimokuwa wamejificha wakiishi bila ya chakula, maji na dawa.