1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atangaza mpango wa kuimarisha miundo mbinu Marekani

John Juma
1 Aprili 2021

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza mpango wa dola trilioni 2.3 kuimarisha miundo mbinu nchini mwake na pia ametangaza kuwa ataongeza ushuru kwa kampuni kubwa ambazo zinalipa ushuru usioridhisha. 

https://p.dw.com/p/3rSes
USA Präsident Joe Biden
Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Rais Joe Biden amesema mpango huo wa kuboresha muundo mbinu ya Marekani utadumu kwa miaka minane na utabuni mamilioni ya nafasi za ajira.

Akizungumza akiwa Pittsburgh jimbo la Pennsylvania, Biden ameongeza kuwa mpango huo utasaidia Marekani kujiimarisha mbele ya China ambayo uchumi wake unakuwa kwa kasi.

Soma pia: Marekani yawaomba washirika wa NATO kuungana dhidi ya China

Miongoni mwa yaliyoainishwa kwenye mpango huo ambayo Biden alitaja kuwa ni wa mara moja katika kizazi ni pamoja na:

Vipaumbele vya mpango huo

  • Kujengwa kwa maili 20,000 ya barabara na kukarabati maelfu ya madaraja.
  • Kuongeza maradufu ufadhili kwa usafiri wa umma na kuanzishwa kwa maelfu ya vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme.
  • Kuongeza ushuru kutoka asilimia 21 hadi asilimia 28 na kuziba mianya kwenye mfumo wa ulipaji kodi.
  • Na kuboresha hospitali, shule na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi.

"Ni lazima tusonge mbele sasa kwa sababu nimeshawishika kwamba tukichukua hatua sasa, katika miaka 50 ijayo watu watatizama nyuma na watasema huu ndio wakati ambao Marekani ilifaulu kuimarisha mustakabali wake.” Amesema Biden.

Soma pia:

Mpango huo utafadhiliwa kwa kuongeza ushuru kwa kampuni na mashirika ya Marekani. Utawala wa sasa wa Marekani unalenga kubatilisha ushuru uliopunguzwa chini ya utawala wa Trump na ongezeko hilo linatarajiwa litagharamia mpango huo kwa muda wa miaka 15.

Ujenzi na ukarabati wa maelfu ya madaraja ni kati ya malengo ya mpango huo
Ujenzi na ukarabati wa maelfu ya madaraja ni kati ya malengo ya mpango huoPicha: Reuters/L. Jackson

Hisia mseto kuhusu mpango huo

Chama cha wafanyabiashara kimeukaribisha mpango huo, lakini kimesema hatua ya kuongeza ushuru ni ushauri hatari. Lakini Biden ameutetea uamuzi wake akisema hata ushuru wa asilimia 28, uko chini ya hali ilivyokuwa mwishoni mwa vita vikuu vya pili duniani na mnamo mwaka 2017.

Aidha Biden ameeleza kwamba yeyote ambaye kampuni yake hupata chini ya dola 400,000 hawataongezewa ushuru, na kwamba suala hilo halikusudii kumuadhibu mtu yeyote kwani hana uadui wowote na mabwenyenye ambao ni mabilionea na mamilionea.

Wakati huo huo ametaja kuwa duka kubwa linalofanya shughuli zake kwa njia ya mtandao Amazon pamoja na mengine kadhaa yaliyoko Marekani kwa sasa hayalipi ushuru kutokana na mapato yao.

Wademokrat ambao wanadhibiti bunge lakini kwa wingi mdogo wamesema wangependa wenzao wa chama cha Republic kuunga mkono mpango huo. Lakini wanaweza kushinikiza mpango huo kupita kama walivyofanya kuhusu mpango wa Biden wa mfuko wa msaada wa dola trilioni 1.9 kukabili athari za janga la COVID-19.

MIongoni mwa malengo ya mpango wa Biden ni kuongeza vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme.
MIongoni mwa malengo ya mpango wa Biden ni kuongeza vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme.Picha: Action Pictures/imago images

Pingamizi dhidi ya mpango huo

Kiongozi wa wachache katika baraza la seneti Mitch McConnell wa jimbo la Kentucky amesema mpango huo kuwa kama njama fiche.

Juhudi za Biden huenda pia zikakumbwa na changamoto kutoka kwa baadhi ya Wademokrat wanaosema hawawezi kuunga mkono ila tu ikiwa utashughulikia matozo ya dola 10,000 yaliyowekwa na utawala wa Trump.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kupitia taarifa ameukashifu mpango huo akisema utakuwa miongoni mwa majeraha makubwa ya kiuchumi katika historia ya taifa hilo. Kulingana na Trump China ndiyo itanufaika akidai kampuni kubwakubwa zitahamia China kwa sababu ya kodi za juu Marekani.

(APE)