Biden ataka ushirikishwaji wahamiaji kupambana na siasa kali | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Biden ataka ushirikishwaji wahamiaji kupambana na siasa kali

Mkutano wa kimataifa jijini Washington juu ya kupambana na siasa kali umefunguliwa rasmi, huku Makamu wa Rais Joe Biden akisema dawa ni kuzijumuisha jamii za wachache kwenye mataifa ya Magharibi.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden.

Mkutano huo, ambao ulianza jana (17 Februari) na unawakutanisha maafisa wa serikali ya Marekani na mawaziri kutoka kote ulimwenguni, unafuatia mashambulizi ya hivi karibuni kwenye miji ya Copenhagen na Paris, ambayo yameirejesha upya dhamira ya mataifa ya Magharibi kupambana na ongezeko la mashambulizi yanayohusishwa na siasa kali.

Lakini akifungua mjadala ulioutangulia mkutano huo kwenye Ikulu ya Marekani, Biden alisema njia muhimu kuliko zote ni kuzifanya jamii zilizo hatarini kuambukizwa siasa kali, kama zile za wahamiaji, kujihisi kuwa ni sehemu ya jamii za wenyeji.

"Tunapaswa kufanya kazi kutoka chini kabisa na kuzijumuisha jamii zetu na kuwafikia wale ambao wanaweza kushukiwa kuwa wamepandikizwa siasa kali kwa sababu wametengwa. Jamii lazima ziwe na njia mbadala kwa jamii za wahamiaji, ziwape fursa, ziwape hisia za kuwa wao ni sehemu ya jamii na tuondoe kile ugaidi unachowapa kupitia hisia za khofu, kutengwa, chuki na kisasi," Biden aliwaambia viongozi wa kijamii na mawaziri waliokutana naye.

Ulaya inapaswa kuwajumuisha zaidi wageni

Kwa mujibu wa Biden, Ikulu ya Marekani inaamini Ulaya imo kwenye hatari kubwa zaidi ya mashambulizi kwa kuwa mara nyingi wahamiaji hujikuta hazijumuishwi ipasavyo kwenye jamii za wenyeji.

Waombolezaji wakikumbuka wahanga wa mashambulizi ya Copenhagen.

Waombolezaji wakikumbuka wahanga wa mashambulizi ya Copenhagen.

Wakikutana mjini Brussels wiki iliyopita, viongozi wa Umoja wa Ulaya walitaka pawepo sheria kali zaidi za kudhibiti wasafiri wanaoingia kwenye eneo la Schengen linalojumuisha mataifa 26 ya Ulaya, na pia ubadilishanaji wa taarifa za wageni kama sehemu ya mkakati wa kupambana na ugaidi baada ya mashambulizi ya Paris.

Kwa upande wake, Uhispania ilipendekeza kufanyiwa marekebisho kwa makubaliano hayo ya Schengen ili kuruhusu upekuzi mipakani, hasa kwa watu wanaoshukiwa kuwa na mafungamano na magaidi, baada ya watu 17 kuuawa kwenye wimbi la ghasia nchini Ufaransa lililoanza na mashambulizi dhidi ya waandishi wa jarida la Charlie Hebdo.

Siku ya Jumapili, polisi katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen, walimpiga risasi na kumuuwa mtu aliyeshukiwa kufanya mashambulizi kwenye sinagogi la Kiyahudi mjini humo na pia kwenye mkutano juu ya uhuru wa kujieleza siku moja nyuma, ambapo watu wawili waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Rais Barack Obama, ambaye hivi leo na kesho ataongoza mkutano huo unaozijumuisha nchi 60 duniani, alituma salamu za rambirambi kwa serikali ya Denmark, na amemualika meya wa mji wa Copenhagen kushiriki mkutano huo. Obama anatazamiwa leo kutoa hotuba juu ya njia bora zaidi za kujenga mustakabali wa dunia usio na siasa kali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com