1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden akutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya

Tatu Karema
15 Juni 2021

Rais Joe Biden wa Marekani anatafuta uungwaji mkono wa Umoja wa Ulaya ili kukabiliana na vitisho kutoka Urusi na China.

https://p.dw.com/p/3uxsB
Belgien Brüssel | USA EU Treffen | Ursula von der Leyen, Joe Biden und Charles Michel
Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

 

Siku ya Jumanne (Juni 14), Biden alikuwa anatafuta uungwaji mkono wa Umoja wa Ulaya huku akikutana na viongozi wa Umoja huo kabla ya mkutano na mwenzake wa Urusi, Vladmir Putin. Viongozi wa Ulaya wana hamu ya kumalizwa kwa vita vya kibiashara vilivyoanza chini ya uongozi wa Trump pamoja na mgogoro wa miaka 17 kuhusu ruzuku ya ndege.

Nini huenda kikajadiliwa?

Biden anatarajiwa kukutana na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Charles Michel, anayewakilisha mataifa ya Umoja huo, na Raiswa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen. Rais huyo amekuwa makini kutafuta uungwaji mkono kutoka barani Ulaya katika juhudi zake za kukabiliana na Urusi kabla ya mkutano wake na Putin siku ya Jumatano (Juni 16) mjini Geneva, Uswisi. Viongozi wote wawili, wa Urusi na Marekani, wameelezea uhusiano kati ya mataifa hayo mawili kuwa mbaya zaidi katika muda wa miaka mingi.

Russland | Präsident Wladimir Putin
Vladmir Putin- Rais wa UrusiPicha: Yevgeny Odinokov/AP Photo/picture alliance

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wako macho kuandaa mazungumzo ya kiwango cha juu na Marekani na Urusi kukabiliana na kile wanachodai ni "ubabe wa Urusi na matamshi ya chuki dhidi ya mataifa ya Magharibi." Mkutano wa Umoja wa Ulaya na Marekani unatarajiwa kujumuisha taarifa ambayo itashughulikia masuala kuhusu mwenendo wa China unaodhaniwa kuwa wa uchokozi. Taarifa hiyo itafuatiwa na nyingine ya kongamano la Jumuiya ya Kujihami ya NATO ambayo ilitangaza kuwa China ni tishio la kudumu katika usalama na kusema kuwa Wachina walikuwa wanafanya kazi kuhujumu mpangilio wa sheria za kimataifa.

Je ni mwisho wa migogoro ya kibiashara?

Viongozi wa Ulaya wanamuona Biden hajashughulikia uamuzi wa Trump wa mwaka 2018 wa kutoza ushuru wa kuingiza vyuma kutoka nje. Pia kuna hamu ya kutatua mzozo wa muda mrefu kuhusu haki ya ruzuku ya serikali ambayo kila upande hutoa kwa kampuni zake kubwa za kutengeneza ndege - ambazo ni Boeing nchini Marekani na Airbus barani Ulaya.
Kabla ya mkutano huo, von der Leyen alisema siku ya Jumanne kwamba alikuwa na imani Umoja wa Ulaya na Marekani zingepata ufumbuzi wa kutokubaliana kwao ambako kumedumu kwa miaka 17.

Biden alianza siku yake kwa mkutano na Mfalme Philippe wa Ubelgiji na Waziri Mkuu Alexander De Croo.