1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aizuru Poland, katika eneo lililo karibu na Ukraine

Daniel Gakuba
25 Machi 2022

Rais Joe Biden amewasili katika mji wa Poland karibu na mpaka wa Ukraine, kuwazuru wanajeshi wa Marekani na kutathmini tatizo la wakimbizi kutoka Ukraine. Urusi yasema awamu ya kwanza ya malengo yake Ukraine imefanikiwa.

https://p.dw.com/p/492uP
Belgien Brüssel | Pressekonferenz Ursula von der Leyen und Joe Biden
Rais Joe Biden akiagana na Ursula von der Leyen mjini Brussels kabla ya kuelekea PolandPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema vikosi vya Urusi vimefanikiwa kuungunisha sehemu ya ardhi kati ya rasi ya Crimea na maeneo ya mkoa wa Donetsk yanayodhibiwa na Urusi. Hata hivyo haikutoa maelezo zaidi.

Rasi ya Crimea ilichukuliwa na Urusi kutoka Ukraine mwaka 2014, na waasi wa mashariki mwa Ukraine wanaoungwa mkono na Urusi wanadhibiti maeneo ya mikoa ya Donetsk na Luhansk, ambayo kabla ya uvamizi wa Urusi, Rais Vladimir Putin aliyatambua kama jamhuri huru.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Marekani Joe Biden anafanya ziara nchini Poland, ambako anawatembelea wanajeshi wa Marekani waliopiga kambi karibu na mji wa Rzeszów ulio mwendo wa takriban saa moja kutoka mpaka wa Ukraine.

Polen Ankunft US-Truppen für Osteuropa
Mji wa Rzeszow wa Poland anaouzuru Rais Joe Biden uko karibu na mpaka wa Ukraine, na una kituo cha wanajeshi wa MarekaniPicha: MACIEJ GOCLON/FOTONEWS/newspix/imago images

Ziara yake hiyo inanua kufanya tathmini ya tatizo la wakimbizi kutoka Ukraine, na kuonyesha mshikamani na nchi hiyo mshirika wa magharibi inayokabiliwa na vita.

Marekani na Umoja wa Ulaya kushirikiana katika sekta ya nishati

Kabla ya kuondoka mjini Brussels mapema leo, Joe Biden alifikia makubaliano na rais wa Halmashauri ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ya ushirikiano katika sekta ya nishati, yatakayoiwezesha Ulaya kuachana na utegemezi wa kawi inayoagizwa kutoka Urusi.

Akizungumza pamoja na Bi von der Leyen, Rais Biden amesema hatua iliyopigwa itaipa Ulaya uhuru wa kutoitegemea tena Urusi.

Ukraine | Zerstörung in Mariupol
Mji wa Mariupol mashariki mwa Ukraine ni mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya zaidi na uvamizi wa UrusiPicha: Nikolai Trishin/TASS/dpa/picture alliance

''Putin alitumia nishati kuzibana na kuzirubuni nchi jirani, na kujiingizia faida anayoitumia kuanzisha vita. Ndio sababu mwezi uliopita nilisimamisha mafuta ambayo Marekani ilikuwa ikiyaagiza kutoka Urusi.'' Amsema Biden na kuongeza kuwa  Marekani inaunga mkono tangazo la Umoja wa Ulaya lenye uzito mkubwa mapema mwezi huu, la kupunguza utegemezi wa gesi kutoka Urusi.

Urusi yasema hatua ya kwanza ya 'operesheni' nchini Ukraine imekamilika

Kwa upande wa Urusi, wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Urusi, Tass kuwa malengo ya sehemu ya kwanza ya inachokitaja kuwa ''Operesheni ya kijeshi'' nchini Ukraine imekamilika.

Shirika jingine la habari la Ifax limeripoti kuwa kunzia sasa Urusi itajikita katika lilichokiita, ''ukombozi kamili'' wa ukanda wa Donbass.

Mchana huu ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu imesema kuwa imekwishathibitisha vifo vya raia 1,081 wa Ukraine, pamoja na wengine 1,707 waliojeruhiwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi.

Imeongeza kusema kuwa inazifnyia uchunguzi taarifa kuwa vifo vya raia wengi zaidi vilitokea katika maeneo yaliyokumbwa na mapigano makali katika mikoa ya Sumy. Kharkiv na Donetsk ambako ndipo uliko mji uliozingirwa wa Mariupol.

rtre,afpe