Biden aishutumu Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Biden aishutumu Urusi

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ameishutumu Urusi kwa kujaribu kuisambaratisha Ukraine na ameonya nchi hiyo inapaswa kuacha kuongea maneno matupu na ionyeshe vitendo vya kupunguza mzozo mashariki mwa Ukraine.

Joe Biden na Arseniy Yatsenyuk

Joe Biden na Arseniy Yatsenyuk

Akizungumza leo mjini Kiev, wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, Joe Biden ameitaka Urusi kuwashinikiza waasi wanaoiunga mkono Urusi, ambao wanaidhibiti miji kadhaa ya mashariki mwa Ukraine, kuweka chini silaha na kuondoka katika majengo ya serikali ambayo wanayakalia pamoja na kwenye vituo vya ukaguzi.

Biden amesema kuwa Marekani iko pamoja na watu wa Ukraine na kwamba Urusi haina haki ya kuiteka nchi jirani na itakabiliwa na vikwazo zaidi na kutengwa, iwapo itaendelea kuuchochea mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Marekani kuongeza juhudi za kuisadia Ukraine

Amesema Marekani inaongeza juhudi za kuisaidia Ukraine kuacha kutegemea gesi kutoka Urusi, kupambana na rushwa pamoja na kujiandaa kwa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Mei 25, mwaka huu.

Kwa upande wake Yatsenyuk amesema kuwa Urusi inapaswa kuzingatia ahadi zake na majukumu yake kimataifa na kwamba nchi hiyo iache kufanya mambo kama majambazi ya karne ya kisasa.

Joe Biden na Oleksandr Turchynov

Joe Biden na Oleksandr Turchynov

Yatsenyuk amesema kuwa vikosi maalum vya Urusi vinaendesha shughuli mashariki mwa Ukraine, kwa lengo la kuuvuruga uchaguzi huo wa urais na ameitaka nchi hiyo kuviondoa vikosi hivyo.

Marekani yaipatia Ukraine Dola Milioni 50

Wakati huo huo, Marekani imeahidi kuipatia Ukraine msaada mpya wa Dola milioni 50 kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.

Fedha hizo zinajumuisha Dola milioni 11 kwa ajili ya shughuli za uchaguzi wa urais. Marekani pia imeahidi kutoa nyongeza ya Dola milioni nane kama msaada kwa jeshi, ikiwemo redio na magari. Msaada huo hautahusisha silaha.

Katika ziara yake hiyo mjini Kiev, Biden amekutana pia na Rais wa mpito Oleksandr Turchynov na wanaharakati wa demokrasia.

Ama kwa upande mwingine, Naibu Kansela wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, ameitaka China kuongeza juhudi katika kusaidia kuutatua mzozo wa Ukraine, ikiwemo kuishawishi Urusi. Gabriel ambaye ni waziri wa uchumi na nishati wa Ujerumani, ameitoa kauli hiyo mjini Beijing, muda mfupi kabla ya kukutana na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com