Bibi Rice azuru Ukingo wa Magharibi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 02.08.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Bibi Rice azuru Ukingo wa Magharibi

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice amekutana rais wa mamlka ya Palestina Mahmud Abbas pamoja na baraza la mawaziri chini ya waziri mkuu Salam Fayyad katika Ukingo wa Magharibi hatua hiyo imeshutumiwa vikali na kundi la Hamas.

Bibi Condoleeza Rice

Bibi Condoleeza Rice

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice kwanza alikutana na waziri mkuu Salam Fayyad kabla ya kutambulishwa rasmi kwa baraza zima la mawaziri, ziara hii inalenga kuonyesha uungwaji mkono wa utawala huo wenye mtazamo kadirifu.

Hii ni ziara ya kwanza ya bibi Rice kwenye eneo la Palestina tangu kundi la Hamas lilipo udhibiti Ukanda wa Gaza.

Kundi la Hamas hata hivyo linapinga utawala wa Ukingo wa magharibi chini ya waziri mkuu Salam Fayyad na kudai kuwa serikali hiyo imenyakuwa tu madaraka ya mamlaka ya Palestina.

Hamas ambayo iliwachishwa kazi na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas pia inamlaumu bibi Rice kwa kuongeza mafuta katika moto unaowaka na kusababisha migawanyiko zaidi miongoni mwa Wapalestina.

Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema kwa mtazamo wake bibi Rice hakuja katika eneo la Palestina kutetea kupatikana taifa huru la Palestina bali amekuja kama ishara ya kumfurahisha tu rais wa Marekani George W Bush.

Baada ya kulihutubia baraza la mawaziri katika Ukingo wa Magharibi waziri wa mambo ya nje wa marekani bibi Condoleeza Rice alikutana pia na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas katika makao yake makuu.

Katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika mkutano wa viongozi hao wawili rais Mahmud Abbas amesema kwamba anafanya kila jitihada kudhibiti hali ya usalama katika eneo la Palestina.

Marekani imetoa msaada wa zaidi ya dola milioni 80 kuvipa nguvu vikosi vya usalama vya Ukingo wa Magharibi.

Bibi Rice amemfahamisha rais wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas kuwa Israel iko tayari kuzungumzia juu ya maswala ya kimsingi na Palestina ili kufanikisha suluhisho la nchi mbili na kwamba wakati huu muafaka ni muhimu kwa Marekani kuutumia ili kufanikisha hayo.

Kabla ya kuzuru Ukingo wa Magharibi bibi Condoleeza Rice alikuwa Jerusalem nchini Israel ambako alikutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje bibi Zippi Livni.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com