Bhutto arejea nyumbani Pakistan baada ya miaka minane uhamishoni | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 18.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Bhutto arejea nyumbani Pakistan baada ya miaka minane uhamishoni

"Tunahitaji demokrasia"-amesema Benazir Bhutto huku machozi yakimtiririka

default

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan,Benazir Bhutto amerejea nyumbani leo asubuhi baada ya kuishi miaka minane uhamishoni.Bibi Bhutto,mwenye umri wa miaka 54 amewasili Karachi ambako umati wa wafuasi wake walimshangiria.

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan alikua kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi.Machozi yakimtiririka.Akiteremka kidogo kidogo ngazi za ndege iliyomleta Karachi kutoka Dubai,bibi Bhutto alisita kidogo kabla ya kukanyaga ardhi ya Pakistan.

“Nimeduwaa,nnafurahi na nna fahari kubwa” alisema bibi Benazir Bhutto ndege yake ilipokua inatuwa katika mji huo wa Karachi wenye wakaazi milioni 12 ambako malaki walikua wakimsubiri na kumshangiria.

“Tunahitaji demokrasia nchini Pakistan-“ameongeza kusema.Viongozi wa serikali ya Pakistan wanaohofia mashambulio ya watu wanayatolea mhanga maisha yao,naiwe wale wanaotumwa na wanamgambo wanaoshirikiana na Al Qaida au wataliban,wamewatuma askari kanzu 20 elfu kulinda usalama.Mwenyewe bibi Bhjutoo anasema tunanukuu:

“Niko tayari na nimekuja kama tulivyopanga.Sijali kitisho cha hatari ya kutaka kuniuwa.Sina wakati wa kupoteza ,nnafikirie jukumu nnalobidi kulitekeleza.”Mwisho wa kumnukuu bibi Bhutto.

Katika wakati ambapo miaka ya nyuma alikua akiahidi atarejea nyumbani ili kukomesha utawala wa kiimla wa jenerali Pervez Musharaff,Benazir Bhuto amerejea nyumbani kama mshirika mkubwa wa rais huyo wa Pakistan.

Kwa mujibu wa wadadisi kadhaa wa masuala ya kisiasa,makubaliano hayo ya hikma kati ya mahasimu wawili wakubwa wa zamani yamewezekana baada ya nasaha ya Marekani kwa rais Musharaff.

Tangu mwezi July uliopita kambi hizi mbili, zinajadiliana namna ya kushirikiana ili kuviwezesha vyama vyao viibuke na ushindi uchaguzi wa bunge utakapoitishwa kati kati ya mwezi January mwakani.

Kuambatana na makubaliano hayo,rais Pervez Musharaff aliyeingia madarakani bila ya umwagaji damu miaka minane iliyopita,na ambae imani ya wananchi kwake inazidi kupungua tangu miezi sita iliyopita,ataendelea kuwa rais na Benazir Bhutto awe waziri mkuu.Serikali ya Marekani inaunga mkono makubaliano kama hayo.

Jenerali Musharaff ni mshirika wao mkubwa katika vita dhidi ya magaidi wa Al Qaida na Washington inaamini wataliban wanaoungwa mkono na wafuasi wa itikadi kali wa kiislam wa Pakistan,wamepiga kambi katika maeneo ya kikabila kaskazini magharibi ya Pakistan-yanayopakana na Afghanistan.

Marekani inaamini ushurikiano kati ya Musharaf na bibi Bhuto utasaidia kuwavunja nguvu wataliban na wafuasi wa itikadi kali ya kiislam nchini Pakistan.Benazir Bhutto,aliyekua kipenzi cha serikali ya Marekani,alipokua waziri mkuu wa Pakistan kati ya mwaka 1988 hadi 1990 na baadae kati ya mwaka 1993 hadi 1996,ameshasema hivi mkaribuni” atawateketeza wafuasi wa itikadi kali na ataruhusu hujuma za madage ya Marekani katika maeneo ya kikabila.”

 • Tarehe 18.10.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77i
 • Tarehe 18.10.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77i

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com