Bernie Sanders amuunga mkono Hillary Clinton | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bernie Sanders amuunga mkono Hillary Clinton

Mahasimu wa kinyang'anyiro cha kugombea tiketi ya kukiwakilisha chama cha Demokrats katika uchaguzi wa Rais nchini Marekani, Hillary Clinton na Bernie Sanders waungana dhidi ya Donald Trump

Hillary Clinton na Bernie Sanders kwenye jukwaa la pamoja

Hillary Clinton na Bernie Sanders kwenye jukwaa la pamoja

Clinton na Sanders walirejea kwenye jimbo la New Hampshire leo kwa mara ya kwanza tangu bwana Sanders amwangushe Clinton vibaya,katika jimbo hilo wakati wa uchaguzi wa mchujo.

Sanders hakusubiri kumwidhinisha aliekuwa hasimu wake kuwa mgombea wa Urais.

Sanders aliichukua hatua hiyo baada ya wiki kadhaa za mazungumzo ili kuziunganaisha nguvu zao zote dhidi ya mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump.

Mkutano wa hadhara wa pamoja baina ya wanasiasa hao wa chama cha Demokrats uliofanyika kwenye shule moja katika mji wa Portsmouth,katika jimbo la New Hampshire, ulikuwa na lengo la kusisitiza umoja wa chama cha Demokrats kabla ya chama cha Republican kumwidhinisha rasmi mgombea wao wa urais,Donald Trump wiki ijayo mjini Cleveland katika jimbo la Ohio.

Katika kumuunga mkono Hillary Clinton Seneta Sanders alitoa mwito wa kuukabili mfumo wa kisiasa na kiuchumi wa kifisadi.

Sanders atoa ujumbe wa kimapinduzi

Wafuasi wa Clinton mjini Portsmouth

Wafuasi wa Clinton mjini Portsmouth

Sanders amesema mfumo huo unawanufaisha matajiri tu.Sanders amemwita Clinton kuwa mgombea wa Urais bora kuliko wengine wote.

Kwenye mkutano wa hadhara wa pamoja wanasiasa hao wa chama cha Demokrats walionyesha umoja dhidi ya mgombea wa chama cha Republican Donald Trump.

Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni ulionyesha kwamba wafuasi wengi wa Bernie Sanders wanapanga kumuunga mkono Hillary Clinton ambae wiki iliyopita aliutangaza,mpango anaokusudia kuutekeleza endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani

Amesema lengo lake ni kujenga uchumi utakaowanufaisha watu wote na siyo wachache tu, walioko juu. Na ndiyo sababu "nautangaza mpango kamambe juu ya kuiweka Marekani mbele katika tekinolojia. Amesema hiyo ni raslimali mojawapo kubwa na anataka wote washiriki.

Clinton anataka tekinolojia itakayoleta nafasi zaidi za ajira. Bibi Clinton pia ameahidi kuchelewesha malipo kwa miaka mitatu, ya mikopo inayotolewa kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Seneta wa jimbo la Vermont Bernie Sanders ameahidi kufanya kila atakaloliweza ili kumzuia Donald Trump kuingia katika Ikulu ya Marekani.

Na uamuzi wake wa kumwidhinisha Clinton unatarajiwa kuwavutia wafuasi wake katika upande wa Clinton pamoja na wale wasiokuwamo katika chama chochote, wale wanaofuata siasa za wastani na wote wengine waliokuwa wanafuata mkumbo katika kumuunga mkono Donald Trump.

Mwandishi:Mtullya abdu.ape/DW

Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com