1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Mgomo wa madereva wa treni wapamba moto

15 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CG1D

Mgomo wa madereva wa treni wa masaa 62 kushinkiza madai yao ya malipo makubwa zaidi ya mishahara nchini Ujerumani umepamba moto kwa kuongezewa na mgomo wa treni za abiria ziada ya ule wa mizigo katika mzozo wa muda mrefu na kampuni ya reli ya taifa Deutsche Bahn.

Mgomo wa treni za mizigo ulianza hapo jana na kukwamisha uchukuzi wa treni za mizigo Ujerumani ya mashariki. Mgomo wa treni za abiria umeanza mapema leo hii na kuwalazimisha abiria wengi kutafuta njia mbadala za usafiri.

Mjini Berlin na katika miji mengine mingi kampuni ya Deutsche Bahn imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa ratiba ya dharura hadi mwishoni mwa juma huku kukiwa hakuna mipango ya kufanya mazungumzo na hakuna suluhisho linaloonekana kwa mzozo huo wa nyongeza ya mishahara.

Wanauchumi wanasema mgomo kwenye reli za mizigo pekee unaugharimu uchumi euro milioni 50 kwa siku na gharama hizo zinaweza kuongezeka hadi kufikia milioni 500 iwapo mgomo huo utadumu kwa zaidi ya wiki moja.

Mgomo huo ambao ni mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya kampuni ya reli ya taifa Deutsche Bahn unatazamiwa kumalizika hapo Jumamosi.