Benoit Hamon kuwania urais Ufaransa kwa tiketi ya Wasoshalisti | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Benoit Hamon kuwania urais Ufaransa kwa tiketi ya Wasoshalisti

Chama cha Kisoshalisti nchini Ufaransa kimemchagua mwanasiasa Benoit Hamon kuwa mgombea wa chama hicho katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

 Mwanasiasa Benoit Hamon alipata nafasi ya kuwakilisha chama cha kisoshalisti katika kinyanganyiro cha nafasi hiyo ya urais baada ya kumshinda mpinzani wake waziri mkuu wazamani Manuel Valls katika uchaguzi wa marudio uliofanyka hapo jana.  Matokeo ya wali yalimpa ushindi a asilimia 58 ya kura Benoit Hamon huku Valls akipata asilimia 42.

Manuel Valls  alikubali kushindwa mara tu baada ya matokeo kutangazwa akisema mwanasisa Benoit Hamon ni chaguo sahihi la chama hicho na kumtakia kila lakheri.

Katika hotuba yake kwa wafuasi wa chama hicho Hamon ambaye anaunga mkono msimamo wa kima maalumu cha chini cha mshahara pamoja huku pia akikusudia kupunguza saa za kazi kwa wiki na kusalia saa 35 alizungumzia pia juu ya hali ya baadaye ya chama hicho.  Mwanasiasa huyo amekuwa pia akiunga mkono suala la kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala.

Waandaaji wa uchaguzi huo wa marudio ambao ulifanyika baada ya wagombea kuchujwa na kubakia wawili walisema idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa ni kubwa ambapo kiasi ya wafuasi milioni 1.3 walijitokeza na hivyo kuongeza hamasa ndani ya chama hicho katika kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Utafiti wa maoni uliofanyika hivi karibuni unaonyesha kumuweka katikanafasi ya tano mgombea wa chama cha Kisoshalisti, akitanguliwa na wagombea wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha far-right National Front Marine  Le Pen, mgombea wa chama cha Independent Emmanuel Macron, mgombea wa chama cha kihafidhina  Francois Fillon na mbunge wazamani Jean-Luc Melenchon.

Wagombea wote wamewahi kushika nyadhifa katika serikali ya Francois Hollande

Präsidentschaftskandidatur Manuel Valls ehemaliger Premierminister reagiert auf vorläufiges (Reuters/P. Wojazer)

Waziri Mkuu wazamani wa Ufaransa Manuel Valls

Wote wawili Benoit Hamon na Manuel Valls  wamewahi kushika nafasi katika baraza la mawaziri la rais wa sasa Francois Hollande ambaye pia ni msoshalisti. Hamon alikuwa ni waziri wa uchumi na baadaye katika kipindi kifupi alikuwa waziri wa elimu wakati Manuel Valls alishika wadhifa wa uwaziri Mkuu katika kipindi cha miaka miwili hadi alipojiuzulu ili aweze kuwania nafasi ya urais. Kupungua kwa umaarufu wa Rais Francois Hollande kumekuwa kukidaiwa kuchangia kupunguza  kwa kiwango flani uungwaji mkono wa chama hicho na tayari rais huyo alitangaza Desemba mwaka jana kutowania tena nafasi hiyo.

Hata hivyo wasoshalisti wanaweza wakafaidika na kashifa inayomuandama hivi sasa mhafidhina Francois Fillon  ambapo mwanasiasa huyo anadaiwa kumlipamshahara mkewe pasipo kufanya kazi, ingawa Fillon mwenyewe amekuwa akikanusha kuwa mkewe alishiriki vikao kadhaa pamoja na kuhudhuria matukio mbalimbali.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais imepangwa kufanyika April 23 na kufuatiwa na hatua ya marudio utakaofanyika May 7  kati ya wagombea wawili watakaopata nafasi ya juu iwapo hakutakuwa na mgombea atakayefikisha kiwango cha kura zinazohitajika katika nafasi hiyo baada ya duru ya kwanza .

Mwandishi: Isaac  Gamba/es/sms (AFP, dpa, Reuters)

Mhariri     :Gakuba Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com