Benki ya dunia yatoa ripoti mpya kuhusu uhamiaji wa wanawake. | Masuala ya Jamii | DW | 27.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Benki ya dunia yatoa ripoti mpya kuhusu uhamiaji wa wanawake.

Benki ya dunia imetoa ripoti mpya juu ya uhamiaji wa kimataifa wa wanawake. Ripoti hiyo inasema nusu ya idadi ya wahamiaji ni wanawake.

default

Uhamiaji wa kimataifa wa wanawake umeongezeka

Wazo kwamba mhamiaji wa kiume huteseka katika nchi ya kigeni kwa niaba ya mke wake na watoto, linahitaji kurekebishwa.

Watu milioni 190, ikiwa ni asilimia tatu ya idadi ya wakaazi duniani, waliishi nje ya nchi walikozaliwa mnamo mwaka wa 2005. Hayo yamesemwa na benki ya dunia ikizinukulu takwimu za Umoja wa Mataifa. Kati ya idadi hiyo, milioni 95 au asilimia 49.6 walikuwa wanawake.

Katika kipindi cha miaka 45 kati ya mwaka wa 1960 na 2005, kiwango cha wanawake katika idadi hiyo kiliongezeka kwa asilimia karibu tatu, kutoka asilimia 46.7, kwa mujibu wa ripoti kuhusu uhamiaji wa kimataifa wa wanawake.

Mwanauchumi wa taasisi ya utafiti wa kimaendeleo ya benki ya dunia, Maurice Schiff, amesema idadi ya wanawake wanaohama kwa sababu ya ajira badala ya sababu za kifamilia, imeongezeka.

Mengi hayajajulikani kuhusu kazi wanayoifanya, pesa wanazopata na kutuma nyumbani na vipi pesa hizi zinavyotumiwa zinapozifikia familia zao. Maafisa wa benki ya dunia wakitumia takwimu rasmi wanakadiria kwamba wafanyakazi wa kigeni hupeleka takriban dola bilioni 200 kila mwaka.

Mwezi uliopita, mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo pamoja na benki ya maendeleo ya Marekani, ziliweka kiwango hicho kuwa zaidi ya dola bilioni 300 kwa mwaka. Haijulikani lakini ni kiasi gani kati ya kiango hiki hupokewa na wanawake.

Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu za hapa na pale na utafiti uliofanywa katika maeneo fulani uliotajwa katika ripoti hiyo ya benki ya dunia, wafanyakazi wa kigeni wanawake huchangia sana kuleta maendeleo katika nchi wanakotokea.

Mwanauchumi wa benki ya dunia katika maswala ya usawa wa kijinsia katika uchumi, Andrew Morrison, amesema wanawake hutuma pesa nyingi kwa familia zao. Ushahidi kutoka maeneo ya mashambani nchini Mexico unaonyesha kwamba uhamiaji wa wanawake husababisha uchumi wa familia wanazoziacha nyuma kuimarika.

Watafiti wamegundua kuwa wanaume katika maeneo ya mashambani ya Mexico yanayokabiliwa na umaskini, sana sana hupanda mazao wanayouza ili kujipatia pesa badala ya kufanya kazi nyingine, wakilinganishwa na wanawake. Kwa hiyo mwanamume anapoondoka kwenda ng ´ambo, familia hupoteza kipato. Anapokuwa ng ´ambo mwanamume analazimika kupata pesa zaidi kuliko zile ambazo angepata akiwa nyumbani kwa ajili ya familia yake, ili aone manufaa ya yeye kufanya kazi ng ´ambo.

Idadi ndogo ya wanawake huondoka kwao kwenda kuishi ng ´ambo, hasa Marekani. Lakini wale wanaokwenda huhitaji kupata pesa kidogo kuliko wanaume ili waweze kuchangia kwa familia zao, kwa sababu nyumbani wanawake hufanya kazi ambazo hazina mishahara, kama vile kukuza mazao kwa ajili ya chakula na kuwalea watoto, miongoni mwa kazi nyingine.

Utafiti umeonyesha kuwa wanaume wanapotuma mishahara yao nyumbani na wanawake kusimamia matumizi yake, kiwango kikubwa hutumika kwa ajili ya elimu na huduma zinaboresha hali ya kimaisha ya familia. Wakati maamuzi ya matumizi ya pesa yanapoachiwa wanaume, kuna hatari ya pesa kufujwa.

Ripoti ya benki ya dunia hata hivyo ina upungufu kwa kuwa takwimu na uchambuzi haujazingatia swala la jinsia. Mirjan Sjoeblom, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo, amesema mojawapo ya ujumbe muhimu wa ripoti hiyo ni kwamba tafiti kuhusu uhamiaji haziwezi kupuuzia wahamiaji wanawake. Ameongeza kusema hii sehemu muhimu ya utafiti kwa kuwa bado kuna maswali mengi ambayo hayajapata ufumbuzi.

Mirjan amesema ipo haja ya kujua zaidi juu ya athari tofauti zinazosababishwa na uhamiaji wa wanaume na wanawake katika familia na masilahi ya watoto, pamoja na kwa nini familia fulani hupendelea uhamiaji wa mwanamke badala ya mwanamume.

Ripoti ya benki ya dunia inasema idadi ya wahamiaji wanawake ni kubwa kuliko ile ya wahamiaji wa kiume katika Sovieti ya zamani, ikifia asilimia 58 na ikiwa inaendelea kuongezeka.

Idadi hii ni sawa na inaongezeka barani Ulaya, Oceania, Amerika Kusini na eneo la Karibik. Ni sawa lakini haiongezeki katika Amerika Kaskazini, na ni ndogo barani Afrika, ikiwa asilimia 47 na inaongezeka. Barani Asia idadi ya wanawake wahamiaji inayokadiriwa kuwa asilimia 43, inapungua.

Nchini Marekani, wanawake kutoka nchi za Karibik, Asia Mashariki, Ulaya na Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, wamejiunga na wafanyakazi kwa idadi kubwa kuliko wanawake kutoka Asia Kusini, Mashariki ya Kati na Afrika Kakazini.

Wahamiaji wanawake waliosomea nchini Marekani hupokea mishahara mikubwa kuliko wanawake waliosoma katika nchi walikozaliwa. Miongoni mwa wanawake waliosoma nchini mwao, wanawake kutoka Ireland, Australia na Uingereza hupokea mishahara mikubwa zaidi.

Miongoni mwa nchi zilizoendelea, wanawake kutoka Afrika Kusini, Jamaica na India wana mishahara mikubwa. Wale kutoka Colombia na Jamhuri ya Dominican na Cuba hupokea mishahara midogo zaidi. Ripoti ya benki ya dunia inasema hii ni kwa sababu hawana ujuzi wa lugha.

 • Tarehe 27.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CTYV
 • Tarehe 27.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CTYV

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com