1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benjamin Mkapa kuzikwa Jumatano Julai 29

24 Julai 2020

Mwili wa rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa utazikwa Jumatano ijayo kijijini kwake, Lupasu, wilayani Masasi mkoani Mtwara.

https://p.dw.com/p/3fsMu
Tansania Benjamin Mkapa Beileidsbuch
Picha: DW/E. Boniphace

Serikali imetenga muda wa siku tatu kuanzia Jumapili hadi Jumanne kuwa ni siku maalumu ya kuaga mwili wa kiongozi huyo aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa. Viongozi mbali mbali wa kitaifa nchini Tanzania wamefika nyumbani kwa marehemu Mkapa, kuipa mkono wa pole familia yake.

Ratiba iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, inaonyesha kwamba shughuli ya kuaga mwili wa kiongozi huyo itafanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam ambako wananchi wa matabaka mbalimbali watapata fursa ya kujitokeza na kumuuga kiongozi wao huyo mpendwa.

Rais Mkapa ambaye katika utawala wake, alisifika kwa kauli mbiu ya uwazi na ukweli atazikwa Jumatano mchana katika kijiji alikoanzia maisha kijiji cha Lupato wilaya ya Masasi.

Wakati huu ambapo Taifa likiwa kwenye maombolezo ya siku saba, salamu za rambirambi zinaendelea kumiminika nchini Tanzania kutoka sehemu mbalimbali, huku baadhi ya viongozi waliowahi kufanya kazi chini ya utawala wake wakikumbusha namna rais huyo alivyolikwamua taifa hili kiuchumi.

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ambaye wakati wa utawala wa Rais Mkapa alikuwa waziri wa mashauri ya kigeni kwa kipindi cha miaka 10, amesema taifa limeondokewa na kiongozi wa aina yake na amewasihi watanzania kuendelea kuyaenzi yale yote aliyoyaasisi

Viongozi watoa ushuhuda kuhusu maisha ya Mkapa

Ratiba ya kuzikwa kwa rais mstaafu Benjamin Mkapa imetolewa na Waziri MKuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Ratiba ya kuzikwa kwa rais mstaafu Benjamin Mkapa imetolewa na Waziri MKuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.Picha: Büro des Premierministers von Tansania

Viongozi wengine mbalimbali wamekuwa wakitoa ushuhuda wao kuhusiana na maisha jumla ya kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alizindua kitabu chake kilichoelezea maisha ya uongozi wake.

Fredrerick Sumaye aliyekuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa Mkapa, amesema utendaji wa kiongozi huyo ulikuwa wa malengo. Sumaye ambaye ni waziri mkuu pekee katika historia ya Tanzania kukaa kwenye wadhifa huo wa kipindi chote cha miaka kumi ameongeza kusema kuwa.

Wanasiasa wa zamani kama mawaziri wakuu wengine wastaafu, mawaziri walistaafu siasa pamoja na wale waliowahi kuwa serikalini wamekuwa wakijitokeza na kumwelezea marehemu Mkapa jinsi alivyokuwa shupavu na mwenye kusimamia maamuzi yake.

Baadhi ya mambo yatayoendelea kukumbwa ni wosia wake aliouacha kupitia kitabu chake ambako amejadili mambo mengi ikiwamo yale yanayohusu mustakabali wa taifa. Moja ya jambo linalizungumzwa sana ni pendekezo lake lililomo kwenye kitabu hicho kuhusiana na haja ya kuwepo kwa katiba mpya.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam