Benghazi yaripuka tena | Matukio ya Afrika | DW | 02.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Benghazi yaripuka tena

Watu 18 wameuawa na zaidi ya 30 kujeruhiwa mjini Benghazi, kufuatia mapigano kati ya jeshi la wanamgambo wa Kiislamu kwenye mji huo wa bandari na kitovu cha mapinduzi ya 2011 dhidi ya Muammar Gaddafi.

Jenerali Khalifa Haftar.Khalifa Haftar

Jenerali Khalifa Haftar.

Kwa siku nzima ya leo (tarehe 2 Juni), mji wa Benghazi umekuwa kwenye taharuki, huku hospitali kwenye mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Libya wakiwaomba watu wachangie damu na wapiganaji kuacha kuwashambulia raia. Kufika jioni hii, tayari wanajeshi 11 na raia saba wameripotiwa kupoteza maisha yao.

"Benghazi inaumia, watu wamechoshwa, waacheni," amesema mkuu wa hospitali kuu ya Benghazi, Dokta Leila Buigiguis, kupitia televisheni ya Libya.

Kwa mujibu wa kamanda mmoja wa jeshi la anga, mapigano hayo yalizuka wakati wa alfajiri pale makundi matatu ya Kiislamu, likiwemo la Ansar al-Sharia, waliposhambulia kikosi maalum cha kijeshi kinachomuunga mkono jenerali mstaafu, Khalifa Haftar.

Kanali Saad al-Werfeli, anayeongoza kikosi cha anga cha Benghazi, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanamgambo walikishambulia kwa mabomu kituo namba 27, na kuwauwa na kuwajeruhi wanajeshi waliokuwa humo.

Ulipizaji kisasi

Watu wakiwa wamekusanyika kwenye Chuo Kikuu cha Benghazi baada ya mashambulizi.

Watu wakiwa wamekusanyika kwenye Chuo Kikuu cha Benghazi baada ya mashambulizi.

Jeshi la anga likajibu kwa kushambulia kwenye vituo vya wanamgambo hao, kwa mujibu wa Werfeli, vikishirikiana na kikosi maalum kinachounga mkono kampeni ya Jenerali Haftar dhidi ya wanamgambo hao mjini Benghazi.

Picha zilizotumwa kwenye mtandao wa intaneti zinaonesha helikopta za kijeshi zikishambulia maeneo yanayoshukiwa kuwa ya makundi ya Waislamu.

Mapigano haya yanatajwa kuwa mabaya zaidi tangu yale ya katikati ya mwezi uliopita, ambapo watu 76 waliuawa katika kile Haftar alichokiita "Operesheni ya Kurejesha Hishima", yenye lengo la kuita Libya mikononi mwa wale anaowaita "magaidi."

Benghazi yazizima

Moshi ukionekana kufuatia mapigano kati ya wanamgambo na wapiganaji wa Jenerali Haftar mjini Benghazi.

Moshi ukionekana kufuatia mapigano kati ya wanamgambo na wapiganaji wa Jenerali Haftar mjini Benghazi.

Wizara ya elimu imefunga skuli na kulazimika kuahirisha mitihani ya mwisho, huku wakaazi wa mji huo wakijifungia ndani na maduka kadhaa yakifungwa pia.

Kwa mujibu wa mashahidi, raia kadhaa wamekwama kwenye kiunga cha magharibi cha mji huo, Sidi Freij, ambacho ni ngome ya kundi la Ansar al-Sharia.

Msemaji wa Jenerali Haftar, Mohamed al-Hijazi, amewatolea wito raia walio kwenye maeneo ya mapigano kuhama na kukimbia Benghazi, hatua inayochukuliwa kuwa ni onyo la wazi kwamba vita huenda vikaendelea kwa muda mrefu ujao.

Tayari tawi la al-Qaida katika eneo la Maghrib limeshatoa wito kwa Walibya kupambana na Haftar na kile anachokiita Jeshi lake la Taifa, na kumuita jenerali huyo wa zamani kama "adui wa Uislamu."

Serikali, makundi hasimu ya wanamgambo na wanasiasa kadhaa wameyakataa mashambulizi ya Jenerali Haftar dhidi ya wanamgambo wakiyaita kuwa ni jaribio la mapinduzi, hasa baada ya wapiganaji kulivamia bunge wiki iliyopita.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza