Bendera ya Marekani yapepea Afrika | NRS-Import | DW | 15.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Bendera ya Marekani yapepea Afrika

Rais George W. Bush ziarani barani Afrika

Rais Bush akiakimkiana na watoto,mwaka 2003 mjini Entebbe Uganda

Rais Bush akiakimkiana na watoto,mwaka 2003 mjini Entebbe Uganda


Mwaka mmoja kabla ya muda wa wadhifa wake kumalizika,rais George W. Bush anaanza hii leo ziara ya wiki moja barani Afrika.Ziara hii ni fursa kwa Marekani kudhihirisha mafungamano yake na Afrika-amesema hayo mshauri wa masuala ya usalama wa taifa katika ikulu ya Marekani,Stephen Hadley,kabla ya rais George W.Bush kuondoka mjini Washington.Lakini uhusiano ukoje hasa kati ya Marekani na Afrika?
Katika ziara yake hii barani Afrika,rais Bush hataki kukabiliana na matatizo,anapendelea badala yake kuwapatia umma wake nchini Marekani picha ya ufanisi na matumaini mema.Ndio maana amechagua kuzitembelea nchi kama vile Ghana,Benin,Liberia,Tanzania na Rwanda ambako mivutano imekwisha,na shughuli za kiuchumi na demokrasia zinanawiri.
Huko rais Bush anaweza kuzungumzia na kuonyesha mafanikio ya sera za Marekani zinazoanza kuleta tija.Nchini Tanzania kwa mfano makubaliano yenye thamani ya dala zaidi ya milioni 700 yanatazamiwa kutiwa saini-fedha zitakazoisaidia nchi hiyo kuyafikia malengo ya Millenium kwa kuupiga vita umaskini.
Suala hapa ni kuonyesha jinsi bendera ya Marekani inavyopepea barani Afrika,anahisi mtaalam mmoja wa masuala ya kisiasa wa kimarekani.Kwasababu kiuchumi na kisiasa,Marekani imeachwa nyuma kabisa na nchi za Umoja wa ulaya na jamhuri ya umma wa China.Marekani inashikilia asili mia 40 tuu ya bidhaa jumla zinazoingizwa na nchi za Umoja wa ulaya barani Afrika na thuluthi moja ya bidhaa hizo inatokea China.Na katika bidhaa zinazosafirishwa na nchi za Afrika,Marekani inapata nusu tuu ya bidhaa jumla zinazoingia katika masoko ya nchi za Umoja wa ulaya. Mafuta kutoka Afrika yanashikilia nafasi muhimu katika shughuli hizo za kibiashara pamoja na Marekani.
Shehena ya mafuta ya Afrika kwa Marekani inatazamiwa kuongezeka toka asili mia 18 hivi sasa na kufikia asili 25 hadi ifikapo mwaka 2015.Kwa hivyo karibu asili mia 80 ya vitega uchumi vya Marekani barani Afrika vinagharimia sekta ya mafuta.Hata hivyo mashindano ya kibiashara ni makubwa pamoja na jamhuri ya umma wa China katika sekta hiyo barani Afrika.
Kiroja ni kwamba Marekani inafanya yale yale yanayofanywa na China katika kuhakikisha itaendelea kupata mafuta.Masuala ya kuendewa kinyume haki za binaadam, vitisho dhidi ya upande wa upinzani na rushwa iliyokithiri,yanafumbiwa macho na pande zote mbili.Si Angola,si Nigeria na wala si Guine ya Ikweta- chemchem mpya ya mafuta katika eneo la mashariki la bahari ya Atlantik.
Wachina lakini wanajijenga zaidi kwa kujenga barabara,njia za reli,hospitali au kwa kuwatunukia wenye madaraka,majumba makubwa makubwa yanayotumiwa kama ofisi za rais na wizara. Si hayo,takriban kila mwaka ,rais au waziri wa mambo ya nchi za nje wa jamhuri ya umma wa China anafika ziarani barani Afrika na mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika umeshaitishwa mjini Beijing.Kwa hivyo China inajulikana zaidi barani Afrika kuliko Marekani ambako mara moja kila baada ya miaka mitano ndipo rais wake anapoamua kulitembelea bara hilo.
Hata katika suala la misaada ya maendeleo China iko mbele ikilinganishwa na msaada wa Marekani ambao sehemu kubwa inatumiwa kwaajili ya kupambana na ukimwi.

 • Tarehe 15.02.2008
 • Mwandishi Räther, Frank / Johannesburg
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D7vF
 • Tarehe 15.02.2008
 • Mwandishi Räther, Frank / Johannesburg
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D7vF
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com