Bemba kizimbani kwa ′kuhonga mashahidi′′ | Matukio ya Afrika | DW | 29.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Bemba kizimbani kwa 'kuhonga mashahidi''

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jean Pierre Bemba amekanusha mashitaka mapya katika mahakama ya ICC ambamo yeye na mawakili wake wanatuhumiwa kuwarubuni mashahidi katika kesi yake kuu.

Makamu wa rais wa Zamani wa DRC, Jean Pierre Bemba akiwa kizimbani

Makamu wa rais wa Zamani wa DRC, Jean Pierre Bemba akiwa kizimbani

Jean Pierre Bemba amesimama kizimbani pamoja na wakili wake Aime Kilolo Musamba, wakituhumiwa kuwapa maelekezo mashahidi na kuwalipa fedha ili wamtetee Bemba katika ushahidi wao, wakati kesi dhidi yake ilipokuwa ikiendelea kati ya mwaka 2011 na 2013.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ya kuwahonga mashahidi ni Jean Jacques Mangenda Kabongo ambaye pia yuko katika kundi la mawakili wanaomtetea Bemba, Fidele Babala Wandu, mwanasheria na mshirika wa karibu wa Jean Pierre Bemba, na Narcisse Arido, shahidi katika kesi kuu inayomkabili Bemba. Wote watano ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na wote wamekana mashitaka dhidi yao.

Bemba na wenzake wamesema malipo yote kwa mashahidi yalilenga kuwawezesha kumudu gharama za ushahidi, na sio kuwashawishi kumpendelea Bemba katika ushahidi wao.

Misingi ya mahakama haina budi kulindwa

Mwendeshamashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda

Mwendeshamashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda

Mwendeshamashtaka Mkuu wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda, amesisitiza kuwa ni lazima kuzilinda kanuni za usawa na haki ambazo ndizo msingi wa kuundwa kwa mahakama hiyo.

Kilolo na watuhumiwa wengine walewekwa rumande kwa muda kwa muda katika mahakama ya ICC, baada ya kukamatwa na vyombo husika katika nchi za Ubelgiji, Ufaransa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hali hiyo iliwafanya mawakili wengine wanaowatetea watuhumiwa katika mahakama hiyo, kulalamika na kuelezea wasiwasi wao kuhusu kitisho kinachowakabili.

Bemba ambaye alikuwa mmoja wa makamu wanne wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa kipindi cha mpito kuanzia Julai 2003 hadi Desemba 2006, amekuwa akikabiliwa na mashitaka katika mahakama ya ICC tangu mwaka 2008, akituhumiwa kusababisha maafa makubwa kwa raia mwaka 2002, wakati wapiganaji wa kundi lake la waasi la Movement for the Liberation of Congo, MLC, walipoingilia kati katika mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Sio hongo, ni ''shukrani''

Jean Pierre Bemba wakati wa kampeni za urais mwaka 2006

Jean Pierre Bemba wakati wa kampeni za urais mwaka 2006

Waendeshamashtaka wamewanukuu mashahidi, na pia mazungumzo ya simu ya wakili Aime Kilolo Musamba ambayo yalirekodiwa, ambamo alijadiliana kuwapa mashahidi euro 50, na kuwaficha mawakili wengine wa Bemba kuhusu suala hilo.

Wamesema Kilolo alisikika akimwambia mmoja wa mashahidi, na hapa nanukuu, '' Hii sio rushwa, ni zawadi ndogo tu kutoka kwa bwana Bemba, kwa sababu umekubali kutoa ushahidi wa kumpendelea''. ,wisho wa kunukuu.

Waendeshamashtaka hao wamesema kuwa katika mazungumzo mengine wakili Kilolo alisikika akimtahadharisha shahidi aliyepokea hongo, kuhakikisha kwamba mawakili wengine wa Bemba ambao ni wazungu hawafahamu chochote kuhusu fedha walizozipokea.

Ikiwa watuhumiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa leo watapatikana na hatia, wanaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha miaka 5 jela, na kutozwa faini ambayo haina kikomo.

Mwaka jana waendeshamashtaka katika mahakama ya ICC ya mjini The Hague walilazimika kuifuta kesi dhidi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye anbatuhumiwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/8, kutokana na kile walichosema ni vitisho vikali dhidi ya mashahidi, pamoja na kuwahonga, hali ambayo ilibainisha changamoto kubwa wanayokabiliana nayo waendeshamashtaka katika mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza