1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUTI:Mlipuko wajeruhi sita katika siku ya pili mapigano Lebanon

22 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzi

Kumetokea mlipuko mkubwa katika eneo linalokaliwa na waislam wa kisunni mjini Beirut huko Lebanon, ambapo inaarifiwa kuwa watu sita wamejeruhiwa.

Mlipuko huo umetokea ukiwa ni katika mfululizo wa siku mbili za mapigano kati ya majeshi ya Lebanon na wanamgambo wa kundi la kipalestina la Fatah al Islam katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina.

Televisheni ya kundi la Hezbollah imesema kuwa mlipuko huo ulitokea kwenye eneo la magari karibu na kituo cha utamaduni cha Urusi.

Hapo siku ya Jumapili mwanamke mmoja aliuawa baada ya kutokea mlipuko kwenye maduka katika eneo linalokaliwa na wakristo.

Majeshi ya Lebanon yameendelea kushambulia wanamgambo wa kipalestina wa kundi la Fatah al Islam waliyojichimbia katika kambi ya wakimbizi wa kipalestina kaskazini mwa Lebanon, karibu na mji wa Tripoli.

Moshi mweusi uligubika anga la kambi hiyo, kutokana na mashambulizi hayo.

Kiasi cha wakimbizi elfu 30 mwa Kipalestina wako katika kambi hiyo, na tayari kiasi cha watu 55 wameuawa katika mapigano hayo.

Kundi la Fatah al Islam ambalo lilijitenga na chama cha Fatah limekuwa likishutumiwa kuwa na maingiliano na kundi la Al Qaida pamoja na mahafidhina wa kisyria.

Vurugu hizo ni mbaya kabisa kuikumba Lebanon toka kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka 1990.

Rais George Bush wa Marekani amelaani vurugu hizo na kusema watu wanaojaribu kusambaratisha demokrasia changa ni lazima washughulikiwe, akiwalenga wapiganaji wa kundi hilo la Fatah al Islam.