1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT:Fouad Siniora aomba kuundwa kwa makahama ya kimataifa

15 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC1z

Waziri Mkuu wa Lebanon Fouad Siniora anatoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuunda mahakama ya kimataifa ili kuwashtaki washukiwa wa mauaji ya Waziri mkuu wa zamani marehemu Rafiq Hariri.Hatua hiyo inadhaniwa kuwa huenda ikazidisha mvutano kati ya serikali inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi na vyama vya upinzani vinavyoongozwa na wapiganaji wa Hezbollah.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano Ghazi Aridi Bwana Siniora aliamuandikia katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon waraka unaotoa wito wa kuundwa kwa mahakama hiyo.Ombi hilo linatolewa baada ya Bwana Siniora kutoungwa mkono na upinzani kuhusiana na suala hilo.

Hatua ya kuundwa kwa mahakama ya kimataifa ili kuwashtaki washukiwa waliotekeleza mauaji ya Rafiq Hariri mwaka 2005 imesababisha mgawanyiko mkubwa nchini Lebanon.Suala hilo linasababisha mkwamo wa kisiasa kati ya serikali na vyama vya upinzani jambo ambalo limesababisha vita vilivyo na misingi ya kidini katika miezi ya hivi karibuni.

Kwa upande mwingine afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa anathibitisha kwamba afisi ya Katibu Mkuu imepokea barua hiyo na inaidurusu.