BEIRUT : Siniora aapa mapinduzi hayatoiangusha serikali | Habari za Ulimwengu | DW | 01.12.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BEIRUT : Siniora aapa mapinduzi hayatoiangusha serikali

Waziri Mkuu wa Lebanon Fouad Siniora amesema hapo jana haton’gatuka kufuatia wito wa kundi la Hezbollah na washirika wake kuitisha maandamano makubwa ya umma mjini Beirut leo hii kujaribu kuilazimisha serikali hiyo kujiuzulu.

Siniora ameliambia taifa kwamba upinzani unataka kufanya mapinduzi dhidi ya mfumo wa demokrasia nchini Lebanon na ameapa kwamba serikali yake inayoipinga Syria haitoanguka.

Amesema katika matangazo yaliyorushwa hewani moja kwa moja na televisheni kwamba hawatoruhusu kufanyika kwa mapinduzi dhidi ya serikali ya utawala wa kidemokrasia,sheria zake na asasi zake na kwamba hakuna njia ya kuipinduwa serikali hiyo isipokuwa kwa kupitia bunge ambalo limeipa serikali hiyo kura ya imani.

Hezbollah na washirika wake wamewataka wananchi wote wa Lebanon kuandamana leo hii kuanzia saa tisa za mchana kuilazimisha serikali hiyo ijiuzulu.

Hezbollah ambayo inaungwa mkono na Syria na Iran inaiita serikali ya Siniora kuwa kibaraka wa Marekani.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com