1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Beijing-Olympic, rekodi ya dunia yavunjwa

Liongo, Aboubakary Jumaa20 Agosti 2008

Michuano ya Olympic inayoendelea huko Beijing leo imeshuhudia rekodi ya dunia ya mbio za mita 200 ikivunjwa, huku mwanariadha wa Ukraine akipatikana na kosa la kutumia madawa ya kuogeza nguvu.

https://p.dw.com/p/F1nQ
Jogoo wa Ethiopea Kenenisa Bekele akishinda mbio za mita 10,000 na kutwaa medali ya dhahabuPicha: AP

Wakati michezo ya Olympic ikiingia katika siku yake ya 13 huko mjini Beijing mshindi wa Medali ya fedha katika mchezo unaoshirikisha michezo aina saba kwa mpigo, Liudmlya Blonska kutoka Ukraine amekuwa mwanamichezo wa kwanza wa ngazi ya juu kubainika kuwa ametumia madawa ya kuongeza nguvu yaliyopigwa marufuku.


Hatua ya kwanza katika vipimo vilivyochukuliwa kutoka kwa mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 30 vimeonesha kuwa alitumia madawa hayo na majibu ya vipimo vya pili yanatarajiwa kutolewa kesho.


Blonska anakabiliwa na kifungo cha maisha Iwapo vipimo hivyo vya pili navyo vitathibitisha kutumia kwake madawa hayo.


Ama kwa upande mwengine Usain Bolt wa Jamaica muda mfupi uliyopita amefanikiwa kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 200 na kutwaa medali ya pili ya dhahabu akitumia muda wa sekunde 19.30 na kumfanya kuwa binaadam mwenye kasi zaidi duniani.


Bolt pia amekuwa mwanariadha wa kwanza katika kipindi cha miaka 24 ya toka Carl Lews wa Marekani alipofanya hivyo kutwaa medali mbili za dhahabu kwa mpigo katika michezo ya Olympic.


Jumamosi iliyopita mwanariadha huyo wa Jamaica alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 100.


Bolt leo amevunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mmarekani Michael Johnson aliyoiweka katika michezo ya Olympic mwaka 1996 huko Atlanta ya sekunde 19 nukta 32.


Naye jogoo wa Ethiopea, Kenenisa Bekele ambaye Jumamosi iliyopita alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita elfu 10,leo usiku anatarajiwa kuwania kufuzu kwa fainali ya mbio za mita 5000.


Mbali naye pia bingwa wa dunia wa mbio hizo Bernad Lagat mzaliwa wa Kenya ambaye anakimbilia Marekani atashiriki, pamoja na Thomas Longoziwa wa Kenya na Moses Kiptui wa Uganda.


Mapema chipukizi Akbel Kiprop aliipatia medali nyingine ya fedha Kenya katika mbio za mita 1500 na alimwambia mwandishi wetu Alex Mwakideu aliyeko huko Beijing ya kwamba..


Sikiliza mahojiano ya Alex Mwakideu na Kiprop