1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Kansela Merkel aendelea na ziara yake nchini China

28 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBUz

Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, ameikosoa China kwa ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habari.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye chuo cha sayansi ya jamii mjini Beijing hii leo, kansela Merkel amezungumzia ukuaji wa kiuchumi na kuishawishi serikali ya mjini Beijing ichukue jukumu kubwa zaidi duniani na iheshimu sheria za kibiashara katika maskono ya kimatiafa.

Haki miliki ni swala kubwa muhimu huku kansela Angela Merkel akiishutumu China kwa kutengeneza motokaa kwa kuigiza miundo ya motokaa za Ujerumani, ambazo zitaonyeshwa kwenye maonyesho ya magari mjini Frankfurt hapa Ujerumani mwezi ujao.

Kampuni za kutengeneza magari hapa Ujerumani, BMW na Smart, zinapania kuzichukulia hatua ya kisheria kampuni za China kwa kupanga kuonyesha magari hayo mjini Frankfurt.

Kansela Merkel amesema China inatakiwa kuchukua jukumu kubwa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, huku ikiendeleza uchumi wake.

´Hiyo ina maana tunalazimika kwa haraka kuleta teknolojia mpya na China inajua kwamba katika siku za usoni itakuwa na jukumu kubwa. Lakini naelewa pia kwamba maendeleo ya kiuchumi lazima yafikiwe.´

Katika siku ya pili ya ziara yake nchini China, kansela Merkel amekutana na waandishi wanne wa habari ambao ni wakosoaji wa sera za serikali ya China.