1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bei ya mafuta yapanda maradufu nchini Kenya

Amina Mjahid
15 Septemba 2021

Wakenya walalamikia bei ghali ya mafuta huku gharama ya maisha ikiwa juu. Wataalam wa uchumi wanalaumu mikakati ya kudhibiti bei hiyo iliyowekwa na taifa hilo na kudorora kwa thamani ya dola, kama chanzo cha hali hiyo.

https://p.dw.com/p/40Mhm
Indien Tankstelle
Picha: Prakash Singh/AFP/Getty Images

Taarifa za kupanda kwa bei ya mafuta mara dufu zimewapata Wakenya wengi na mshangao.

Bei ya mafuta imefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya. Bei ya mafuta ya petrol sasa ni shillingi 134.72 baada ya kuongezeka kwa shilingi 7.58. Bei ya mafuta ya dizeli imeongezeka kwa 7.94 na ya mafuta ya taa imepanda kwa shilingi 12.97.

Serikali ya Kenya imesema ongezeko hili limesababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia. Mamlaka ya kitaifa ya kudhibiti mafuta na nishati ina utaratibu uliopitishwa na bunge inayotumia kudhibiti bei ya mafuta na nishati.

Thamani ya dola na mahitaji ya mafuta na mikakati ya ushuru ya taifa vinaathiri pakubwa bei ya mafuta nchini Kenya. 

Kufuatia hatua hii mfumuko wa bei ya bidhaa unatarajiwa nchini, nao wahudumu wa magari ya uchukuzi wakidai watapandisha gharama ya nauli. Kwenye mitandao ya kijamii Wakenya wamelalamikia hali hii siku nzima, wakiwakosoa viongozi wa kitaifa kwa kushindwa kuzuia kuteseka kwa Mkenya wa kawaida.

Tangazo hili linaashiria hali ngumu ya maisha inayowakodolea macho Wakenya wengi ambao bado wanang'ang'ana kujikwamua kutokana na athari za janga la COVID 19.

Mwandishi: Wakio Mbogho, DW, Nakuru