1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yapaa juu, Leipzig yayumba

Bruce Amani
20 Machi 2017

Tunaanza na Bundesliga ambapo Bayern Munich waliupanua uongozi wao kileleni mwa ligi kuu hadi pointi tatu baada ya Thomas Muller kufunga goli pekee katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya wenyeji Borussia Moenchengladbach

https://p.dw.com/p/2ZZLQ
Deutschland Borussia Mönchengladbach v Bayern München
Picha: Reuters/T. Schmuelgen

Ni ushindi wa sita mfululizo kwa Bayern katika mashindano yote ambapo walionekana kuutawala mchezo kwa asilimia 70. Lilikuwa bao la pili la Muller msimu huu na lake la kwanza tangu desemba mwaka jana lakini amegeuka kuwa mtoa pasi 11 zilizopelekea kufungwa mabao. Huyu hapa Mueller "Inafuahisha sana kwamba tumeshinda. Pia nimeweza kufunga bao, hiyo bila shaka inafurahisha. Tumeburudika. Ulikuwa mchuano mkali. Kwa hivyo leo jumapili jioni ntakuwa hoi. Watu wengine watakuwa katika hali ya kutulia. Bila shaka lazima tukutane".

Wenyeji Gladbach, wameteremka hadi nafasi ya 10 baada ya kichapo hicho. Mapema jana, Schalke 04 ilipanda nafasi mbili juu hadi ya tisa baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mainz. Sead Kolasinac alipachika wavuni bao hilo la ushindi. "Tulijitahidi sana kusogea nafasi za Europa League na kushinda mechi ya Bundesliga kabla ya kujiunga na timu ya taifa. Sasa tunaweza kujiunga na timu ya taifa kwa mechi za kimataifa bila shinikizo kabla ya kuendelea katika wiki mbili zijazo".

Deutschland Borussia Mönchengladbach v Bayern München
Thomas Müller alifunga bao lake la pili msimu huuPicha: Reuters/T. Schmuelgen

Nambari mbili kwenye ligi RB Leipzig waliendelea kusambaratika baada ya kufungwa 3-0 na Werder Bremen siku ya Jumamosi. Kocha Ralph Hassenhtul amesema ni vyema kukitumia kipindi kinachoanza wiki hii cha michezo ya kimataifa kujinoa makali kabla ya kuanza kupambana katika mkondo wa mwisho wa ligi. Kichapo hicho kimewaacha katika nafasi ya pili na pointi 49, ikiwa na tofauti ya pointi tatu mbele ya Dortmund

Wakati huo huo Cologne waliimarisha nafasi zao za kucheza kandanda la Ulaya msimu ujao baada ya kuwamiminia mabao manne kwa mawili Hertha Berlin wanaoshikilia nafasi ya pili. Peter Stöger ni kocha wa Köln "Nna furaha kubwa sana kwamba tumecheza vizuri sana dhidi ya mpinzani mkali kabisa ambaye kila mara alikuwa hatari sana. Tulikuwa na nafasi ambazo tungeweza kufunga mabao zaid. Tumeona tulichotaka, kuwa wajasiri na matumaini ndani yetu na kushiriki kikamilifu katika mchezo huo na kujaribu kujikinga. Tulitekeleza vyema kile tulichozungumza".

Deutschland Werder Bremen - RB Leipzig | Marcel Sabitzer
Mambo hayawaendei vyema vijana wa LeipzigPicha: picture alliance/dpa/C. Jaspersen

Ni mechi iliyokuwa muhimu sana kwa mshambuliaji Anthony Modeste aliyetikisa nyavu mara tatu.

Modeste sasa ana mabao 22 nyuma ya Mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang ambaye alifunga bao lake la 23 katika ushindi wao wa Ijumaa usiku wa 1-0 dhidi ya Ingolstadt. Robert Lewandowski ni wa tatu akiwa na mabao 21.

Wolfsburg waliwafunga washika mkia Darmstadt 1-0 wakati nambari nne Hoffenheim walipata ushindi wa 1-0 na sasa wako nyuma ya nambari tatu Borussia Dortmund na tofauti ya pointi moja pekee. Julian Nagelsmann ni kocha wa Hoffenheim "Leverkusen ina timu nziri sana, yenye wachezaji wa bei ghali na hivyo bado hawajatimiza matarajio yao. Lakini bado ni timu kubwa katika Bundesliga. Na hilo pia nimewaambia wachezaji wangu na mtu anaweza kuona. Katika kipindi cha kwanza tulikuwa ovyo  na mchezo wetu haukuwa sawa. Katika kipindi cha pili, tulijipanga vyema na tukapata bao safi"

Vita vya juu ya eneo la kushushwa ngazi vimepamba moto ambapo timu nne zina pointi 29. Timu hizi ni Mainz, Werder, Augsburg na Wolfsburg. Hamburg ni ya tatu kutoka nafasi ya mkia. Ingosltadt na Darmstadt  sasa zinakodolea macho shoka la kushushwa ngazi huku zikiwa zimesalia mechi 9 msimu kukamilika.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdulrahman