1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yanyakua ubingwa wa mataji mawili ya msimu

Sekione Kitojo
27 Mei 2019

Bayern Munich yasherehekea ubingwa wa  pamoja  wa Ligi na kombe la  shirikisho kwa mara ya 12, nchini Ujerumani

https://p.dw.com/p/3JDCm
München - FC Bayern München feiern den DFB Pokalsieg am Marienplatz
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Beier

Sherehe  rasmi  za  ubingwa  wa  Bundesliga  pamoja  na kunyakua  ubingwa  wa  kombe  la  shirikisho  kwa  Bayern Munich hapo  jana  mjini  Munich. Mashabiki  wa  Bayern Munich walisherehekea  ushindi  wa  mabao 3-0 dhidi  ya  RB Leipzig  jana, ushindi  ambao  umewapatia  mabingwa  hao  kombe  hilo  la  DFB Pokal  kwa  mara  ya  19  na  kuwezesha  kukamilisha  ushindi  mara mbili  wa  ligi  pamoja  na  kombe  kwa  pamoja  katika  msimu mmoja. Maelfu  ya  mashabiki  wa  bayern  waliujaza uwanja  wa Marienplatz  mjini  Munich  kwa  kuimba nyimbo  na  kucheza  katika sherehe  hiyo pamoja  na  kikosi  cha  Bayern Munich kilichofanikisha  hatua  hiyo  wakijitokeza pamoja  na  mataji  hayo mawili.

München - FC Bayern München feiern den DFB Pokalsieg am Marienplatz
Mashabiki wa Bayern Munich wakisherehekea ubingwa wa mataji mawili ya ndani, Ligi na kombe la DFBPicha: Getty Images/Bongarts/A. Beier

Ni mara ya  12  kwa  bayern  kupata  ushindi wa mataji  mawili katika  msimu  mmoja  wakati  kocha  Niko Kovac , ambaye alinyakua  ubingwa  wa  kombe  hilo  akiwa  na  Eintracht Frankfurt msimu  uliopita na  kuiongoza timu  hiyo  kuingia  fainali  katika mwaka  2017, amekuwa  mtu  wa  kwanza  kushinda  mataji  mawili na  Bayern  akiwa  mchezaji  na  pia  kama  kocha.

Akiwa  katika  baraza  ya juu  ya  jengo ilipofanyika  sherehe  hiyo kocha Niko Kovac  aliwashukuru  wafuasi  wa  Bayern  kwa  kusema:

"Hatimaye  lakini  sio  mwisho, napenda  niwashukuru  nyie wote. Nyie , ambao  wiki  baada  ya  wiki  mmetufuata ikiwa  nyumbani ama  nje ya hapa. Tumekuwa  na  nyakati  ngumu  lakini, lakini mmetuunga  mkono, katika  nyakati  mbaya  na  nzuri. Mlikuwa  kila wakati nasi. Hatungeweza  kufanikiwa  bila  nyie, na  jana  pia tusingefanikiwa. Ndio sababu  nasema  tunawashukuru  sana. Bakini kama  mlivyo. Nawapenda na  nawatakia  kila  la  kheri."

München Marienplatz Meisterfeier FC Bayern Lewandowski
Robert Lewandowski akiwa pamoja na mataji yote mawiliPicha: Getty Images/Bongarts/A. Beier

Mashabiki  pia  walipata  fursa ya  kuwaaga Frank Ribery  ambaye amecheza  kwa  mara  ya  mwisho  dhidi  ya RB Leipzig akiwa  na klabu  hiyo, na  Arjen Robben , ambao  wote  wanaondoka  kutoka katika  kikosi  hicho. Ribery  alisema.

"Tumeshinda  pamoja  na  mnafahamu, itabaki  kuwa  hivyo  milele, hatuwezi  kusahau kile  tulichokifanya kwa pamoja. Ahsante kwa kila kitu, asante kwa  timu yangu. Nawapenda. Asanteni  sana."

Nae  Arjen Robben, akiwaaga  mashabiki  wa  FC Bayern  alisema:

"Ningependa  tu kuwashukuru.  Ilikuwa  miaka  10 ya mafanikio. Tumesherehekea  mataji  mengi  pamoja. Tulipata mafanikio makubwa. familia  yangu  na  mimi  tumejisikia  tuko  nyumbani  hapa tangu  siku  ya  mwanzo  na  kwa  hiyo  nawashukuru  na nitaendelea  kuwa  mmoja  wetu."

Bundesliga 34. Spieltag | FC Bayern München - Eintracht Frankfurt | Meisterschaftsfeier Bayern
Wachezaji wa Bayern wakiwa na ngao ya ligi nchini UjerumaniPicha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Wakati  huo  huo  rais wa  Bayern Munich  Uli  Hoeness ameonesha kumuunga  mkono  kocha  Niko  Kovac na  kumshauri mlinzi  wa  kati wa  Bayern Munich Jerome Boateng  kutafuta  klabu  nyingine wakati  wa sherehe za  ubingwa  wa  ligi  na  kombe  la  shirikisho mjini  Munich  jana  Jumapili. Ushindi  huo umeondoa  tetesi kuhusiana  na  Kovac, kwamba  huenda  kibarua  kikaota majani baada  ya  kufanya  vibaya  mwanzoni  mwa  msimu  huu.

Akiulizwa  iwapo  Kovac , ambaye  ana  miaka  mingine  miwili  zaidi katika  mkataba  wake  baada ya  msimu wake  wa  kwanza akiwa Bayern, atakuwa  kocha msimu ujao, Hoeness  alijibu ; " kwa asilimia  100, ndio."

Lakini Hoeness  ameweka  wazi  kwamba klabu  hiyo  inatarajia mengi  kimataifa baada  ya  Bayern  kutupwa  nje  ya  Champions League  dhidi  ya  Liverpool  katika  mchezo  wa  timu 16 zilizobakia katika  Champions League.

DFB Pokal Finale - RB Leipzig vs Bayern München | Niko Kovac
Niko Kovac akipokea kombe la DFB PokalPicha: Reuters/W. Rattay

Hoennes  hata  hivyo  amesema  Boateng  mwenye umri  wa  miaka 30 , ambaye  hakutumika  siku  ya  Jumamosi  katika  mchezo  wa kombe  la  Ujerumani  na  sio  tena  chaguo la  kwanza  chini  ya kocha  Nico Kovac , anapaswa  kutafakari  kuondoka  klabuni  hapo licha  ya  kuwa  na  mkataba  hadi mwaka  2021.

Bayern Munich  kwa  hiyo  itakutana  na  Borussia  Dortmund  katika kombe  la  Super Cup msimu  ujao hapo Agosti 3 , limesema shirikisho linaloendesha  ligi  ya  Ujerumani DFL leo Jumatatu.