Bayern yaelekea kutwaa ubingwa wa saba Bundesliga | Michezo | DW | 06.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bayern yaelekea kutwaa ubingwa wa saba Bundesliga

Bayern  Munich  hatima ya ubingwa  wa  Bundesliga  iko mikononi mwao, wakati Borussia  Dortmund  yategemea  miujiza kunyakua ubingwa.

Bayern Munich imejisogeza  karibu  na  ubingwa  wake  wa  saba  mfululizo  katika Bundesliga wakati  imebaki  michezo  miwili baada  ya  kufungua mwanya  wa  pointi  nne  dhidi ya  Borussia  Dortmund kwa  ushindi wa  mabao 3-1 dhidi  ya  Hanover 96. Borussia  Dortmund iliteleza pale  ilipolazimishwa  sare  ya  mabao 2-2  dhidi  ya  Werder Bremen siku  ya  Jumamosi.

Fussball Bundesliga l SV Werder Bremen vs. Borussia Dortmund (Getty Images/O. Hardt)

Maximilian Eggestein wa Bremen akiumiliki mpira karibu na mchezaji wa BVB Thomas Delaney

Frank Ribery ataondoka Bayern  Munich mwishoni mwa  msimu lakini mwishoni  mwa  juma  lijalo anaweza  kuwa  mchezaji pekee katika  Bundesliga  katika  historia akiwa  na mataji  tisa katika  jina lake.

Mfaransa  huyo  mwenye umri  wa  miaka 36, ambaye  alijiunga  na Bayern mwaka  2007, ameshinda  mataji  makubwa  21 akiwa  na Bayern. Kwa  ushindi  dhidi  ya  RB Leipzig  Jumamosi  ijayo anaweza kuondoka  akiwa  na  mataji tisa.

Pizzaro mchezaji mkongwe

Mchezaji  wa  Werder Bremen  Claudio Pizzaro alipachika  bao  dhidi ya  Borussia  Dortmund  baada  ya kuingia  uwanjani  akiwa mchezaji  wa  akiba. Ni bao la  20  la  mshambuliaji  huyo  mwenye umri wa  miaka  40  akiwa  mchezaji  wa  akiba, likimuweka  nyuma tu ya  mfungaji bora wa muda  wote Nils Petersen wa  Freiburg.

Fussball Bundesliga l SV Werder Bremen vs. Borussia Dortmund (Getty Images/O. Hardt)

Mshambuliaji Claudio Pizarro (katikati) akishangilia bao lake dhidi ya Borussia Dortmund

Bayer Leverkusen wameshinda  michezo minne  mfululizo, kiwa  ni pamoja  na  mchezo wao  wa  jana  Jumapili ambapo waliirarua Eintracht Frankfurt  ambao ni timu inayowania  pia  kucheza  katika Champions League  msimu  ujao kwa  mabao 6-1, na  kuwa sawa kwa  pointi  katika  nafasi  ya  tano  ya  ligi wakipambana  kuwania kungia  katika  timu  nne  bora  za  Bundesliga.

Ni mara ya kwanza  kwa  Leverkusen  kupachika  mabao 6  katika nusu  ya  kwanza  ya  mchezo katika  ligi.

Katika  Bundesliga  wakati  huu  ikiwa imesalia michezo miwili  ligi kumalizika, kuna mpambano  wa  kuwania  kuingia  katika  timu  nne bora ambazo zitakuwa  na  fursa  ya  kucheza  katika  Champions League msimu  ujao na  pia  kuna  vuta nikuvute  wa  kuwania ubingwa.

Bayern Munich imefungua  mwanya  wa  pointi nne  dhidi ya  Dortmund  lakini  kinyang'anyiro  hicho  hakijamalizika kwani Borussia  Dortmund inasema  lolote linaweza  kutokea  na  Bayern ikateleza  kama  ilivyoteleza  yenyewe mwishoni  mwa  juma  hili kule Bremen..

Fussball Bundesliga l Schalke 04 vs FC Augsburg l Suat Serdar (Getty Images/Bongarts/L. Baron)

Mchezaji wa Schalke 04 Suat Serdar akishangaa kukosa bao

Schalke yasuasua

Schalke 04 imefanya  vya  kutosha  kupata  sare  ya  bila  kufungana dhidi  ya  Augsburg kujihakikishia  kubakia  katika  ligi  daraja  la kwanza Bundesliga  licha  ya  msimu  uliojaa  matatizo. Lakini  ni mara  ya  nane  wanashindwa  kupata  bao katika  mchezo  wa nyumbani  msimu  huu, ikiwa  ni  mara  nyingi  zaidi  ya  misimu mingine  ya  Bundesliga. Wameshindwa  pia  kushinda  katika michezo  saba  ya  nyumbani , ikiwa  ni  rekodi  yao  mbaya  kabisa tangu  mwaka 1992.